Viwanja vya Namfua, Jamhuri Mkwakwani vyafungiwa

NA ZAINAB IDDY

BODI ya Uendeshaji ya Ligi Tanzania (TPLB), imefungia viwanja vitano kutokana na usalama mdogo kwa mashabiki na kutokidhi vigezo.

 Akizungumza na Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu TPBL, Boniface Wambura, alisema viwanja hivyo vinakosa sifa ya kutumika kwa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.  

Alitaja viwanja vilivyofungiwa ni Jamhuri mkoani Morogoro, unaotumiwa na Mtibwa Sugar Namfua (Singida United) na Mkwakwani, Tanga (Coastal Union) kwa michezo ya Ligi Kuu Bara.

Viwanja vingine vilivyofungiwa ni Bandari, Temeke na Kinesi, Kinondoni vinavyotumika kwa Ligi Daraja la Kwanza Bara.

Wambura alisema viwanja vya Bandari na Kinesi havina usalama kwa mashabiki, lakini sehemu ya kuchezea (pichi) inahitaji kufanyiwa matengenezo.

Alisema viwanja wa Jamhuri, Namfua na Mkwakwani, pichi yake si nzuri na watumiaji wanatakiwa kufanyia matengenezo.

Wambura alisema kikao cha bodi kilichofanyika Oktoba 7, mwaka huu, kilipitia masuala mablimbali ukiwamo la ukaguzi wa viwanja.

“Katika kikao hiko, bodi imeamua kukifungia kiwanja cha Jamhuri, Namfua na Mkwakwani hadi pale watumiaji wake watakapovifanyia matengenezo katika sehemu ya pichi.

“Lakini pia bodi imevifungia viwanja vinavyotumiwa na timu za Ligi Daraja la Kwanza ambavyo ni Kinesi na Bandari tatizo lake ni sehemu ya pichi na usalama kuwa mdogo kwa watazamaji.

Wambura alisema: “Tayari tumeshatoa taarifa kwa watumiaji wake wanatakiwa kuvifanyia ukarabati au kutoa taarifa ya kubadilisha viwanja ambavyo vitakaguliwa na kupitishwa kwa mechi zinazokuja.” 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*