UKAME WA MABAO CHELSEA WAMTESA OLIVIER GIROUD

LONDON, England


BAADA ya mshambuliaji wa Man United, Alexis Sanchez, kuweka wazi kinachomkosesha raha msimu huu, naye straika wa Chelsea, Olivier Giroud, amekiri kuwa ukame wa mabao unamnyima amani moyoni.

Giroud alisema tangu atue Chelsea akitokea Arsenal, ukame wa mabao unamkosesha raha.

Mfaransa huyo alitua Stamford Bridge akitokea Emirates, mapema Januari, mwaka huu, kwa dau la uhamisho la pauni milioni 18, kwa lengo la kuongeza kiwango kitakachompatia nafasi timu ya Ufaransa inayoshiriki Kombe la Dunia msimu huu.

Giroud amekutana na vita kali ya kuwania nafasi kikosi cha kwanza cha Chelsea dhidi ya Eden Hazard na Alvaro Morata.

Straika huyo ameifungia Chelsea bao moja tu hadi sasa, akifanya hivyo katika ushindi wa mabao 4-1 walioupata dhidi ya Hull City.

Hilo la kufunga bao moja katika mechi 10 ndilo linalomkosesha usingizi Giroud na alikiri kuwa hana budi kuboresha makali yake mbele ya lango.

“Kinachonipa nguvu ni kwamba nimeshazoea maisha ya Chelsea, walinikaribisha vyema na tunashirikiana ipasavyo uwanjani,” alisema Giroud.

“Lakini, kazi yangu ni kufunga mabao. Ilibidi niwe na mabao ya kutosha hadi sasa, takwimu zangu zinaangaliwa kwenye mabao. Ukiangalia, bado nimeganda kwenye bao moja na asisti tatu katika mechi tano za Ligi Kuu.

“Bado sijaridhika. Lakini kiujumla inanitia moyo. Muda si mrefu nitarudi kwenye makali yangu. Kama mchezaji, huna budi kujitambua mwenyewe,” alisema.

Giroud alikiri kuwa, si kazi rahisi kuzoea mazingira mapya haraka, hasa unapohama timu moja kwenda nyingine ndani ya mwezi Januari.

“Ukihama Januari, si rahisi kuzoea timu mpya haraka. Lakini nilitamani sana kuwa kwenye kiwango chake hata kama ndio kwanza nilitoka kupona baada ya wiki sita.

“Kocha (Antonio Conte), alinianzisha katika mechi ya pili dhidi ya West Brom (waliyoshinda 3-0) na nilijisikia vizuri.

“Nilicheza vyema, lakini nilitakiwa kuwa na kiwango chenye mwendelezo. Lakini, kiujumla, narudia tena, maendeleo yangu yananipa moyo,” aliongeza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*