googleAds

Tusisahau tuna michuano ya CHAN

LIGI Kuu Bara inaendelea kushika kasi huku ratiba ikionekana kubana lengo likiwa msimu wa 2019/20 imalizike kwa muda uliopangwa.

Kwa mechi za hivi karibuni waamuzi wamekuwa wakimulikwa kutokana na maamuzi tata ikiwemo kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea. Malalamiko hayo yamefika serikalini na tayari waziri mwenye dhamana ya michezo imetaka Baraza la Michezo Tanzania kutoa maelezo.

Aidha kilio cha waamuzi kuboronga imeifikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Rais wake Wallace Karia ameielekeza Kamati ya Waamuzi kukutana na Bodi ya Ligi kutathmini kuhusu mwenendo wa uchezaji wa waamuzi. Katika kikao hicho, Karia alisema watakwepo baadhi ya maafisa wa TFF kutoka idara ya mashindano.     

BINGWA tunaamini suala la waamuzi kuboronga litapata ufumbuzi kwa sababu waamuzi ni sehemu ya mafanikio ya soka la nchi. Tunataka kuona waamuzi wetu hawaishi kuchezesha tu mechi za Ligi Kuu Bara mbali wanaitwa kuchezesha mechi za kimataifa kama michuano ya Afrika ngazi ya klabu, Kombe la Afrika na Kombe la Dunia.

Wakati ligi inaendelea tusisahau kwamba tumefuzu michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani maarufu CHAN ambazo fainali zake zimepangwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini Cameroon.

BINGWA tunaamini kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, anafuatilia kwa karibu ligi yetu ili apate wachezaji ambao watailetea heshima nchi kwa michuano ya CHAN tutakayoshiriki kwa mara ya pili.

Hatutaki kuona wachezaji wale wale licha ya kwamba viwango vya vimeshuka na hawajakuwa na msaada kwa timu zao. Hamna ubishi Simba, Yanga na Azam FC ni miongoni mwa timu kubwa nchini zinazotarajiwa kutoa wachezaji wengi katika kikosi cha Taifa Stars.

Lakini kwa wafuatiliaji wa mechi kadhaa za Ligi Kuu Bara msimu huu, wachezaji wa timu zingine wamekua wakionyesha kiwango kizuri. Ndayiragije na benchi lake la ufundi watahitajika kuwa makini watakapoteua kikosi chao ili kupunguza malalamiko.

Kwa wachezaji nao ambao wana ndoto wa kuiwakilisha taifa kwenye michuano ya CHAN, tunawataka wapambane katika ligi inayoendelea na hususan kuepuka kupata majeraha yatakayo waweka nje ya uwanja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*