googleAds

TUNAMPENDA

NA ZAINAB IDDY

HII unaweza kuiita zawadi ya ‘Valentine Day’ na hakuna atayekuuliza. Ni mapokezi ya kibabe aliyoyapata kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, wakati timu hiyo, ikiwa njiani kuelekea mkoani Iringa.

Wekundu wa Msimbazi watashuka dimbani kesho kupepetana na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ni baada ya kuwachapa Mtibwa Sugar mabao 3-0, Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Wakielekea Iringa jana, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi waliokuwa kwenye msafara huo walilazimika kuweka kituo Mikumi, Morogoro, kutokana na wingi wa mashabiki waliokuwa njiani.

Huku kambi hiyo ya muda mfupi ikiwapa mashabiki fursa ya kupiga picha na wachezaji wao, pia ilishuhudia kuzinduliwa kwa tawi jipya, Simba wa Mikumi.

Wakiwa Mikumi, jina la Sven ndilo lililokuwa limetawala midomoni mwa mashabiki, wengi wakitaka kupiga naye picha, huku waliokosa nafasi hiyo wakitamani walau kumpa mkono.

Mapokezi hayo ya kishujaa yamekuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu Wekundu wa Msimbazi walipoisambaratisha Mtibwa Sugar.

Kabla ya matokeo hayo, Sven alikuwa akitabiriwa kufukuzwa kazi kutokana na ushindi kiduchu wa timu, sambamba na kikosi chake kucheza soka lisilovutia.

Hata hivyo, kwa kilichotokea jana Mikumi, ni wazi mashabiki wa Simba wamesahau yote, kwamba sasa wako tayari kumuunga mkono Mbelgiji huyo.

Mbali ya Sven, mlinda mlango Aishi Manula naye ‘alikusanya kijiji’ kutokana na ushawishi wake, ambapo wapo waliopiga naye picha, ukiacha idadi kubwa ya waliokuwa wakilitaja jina lake.

Haijasahaulika kuwa Manula alikuwa shujaa katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, kwani licha ya kusugua benchi tangu walipocheza na Yanga (Januari 4, mwaka huu), hakuonekana kupoteza hali ya kujiamini langoni.

Akizungumza kutoka Mikumi mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Tawi la Simba wa Mikumi, Ally Lipunguti, alisema wanachama na mashabiki wa timu wamefurahi kuona kikosi choa kimesimama kwa muda kufungua tawi na kuzungumza.

“Tumefurahi sana na hii ni bahati ya pekee kwa mashabiki wa Simba Mikumi. Kwanza tumekutana uso kwa uso na kocha ambaye awali hatukuwahi kuonana naye. Pili, tumezungumza na wachezaji na kuwaambia mambo gani wanayafanya na kutuumiza.

Lipunguti alisema ili kuonesha wapo pamoja, tawi lao limekabidhi katoni 20 za maji na kuwataka wachezaji wajitume ili kuipa ushindi timu hiyo.

Wakati huo huo, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, ameliambia BINGWA jana kuwa kikosi chao kimewasili salama mkoani Iringa na kesho kitafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuikabili Lipuli FC.

“Tumewasili Iringa majira ya jioni na wachezaji wanapumzika, kisha kesho (leo) tutafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuwakabili Lipuli Jumamosi.

“Wachezaji wote wapo salama, hata wale waliokuwa wagonjwa, hivi sasa wapo pamoja na wenzao. Tunamwachia kocha angalie nani atampa nafasi kulingana na mchezo husika. Lakini nina uhakika tuna nafasi ya kupata pointi tatu,” alisema Rweyemamu.

Katika mchezo wa kesho, wenyeji Lipuli wana kibarua kizito cha kupindua meza kwani katika mchezo wa raundi ya kwanza katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, walitandikwa mabao 4-0 na Simba.

Simba wameng’ang’ania kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 53 walizovuna katika mechi 21, ambapo wameshinda 17, wamefungwa mbili na kutoa sare mbili.

Previous Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*