Tshabalala kama ananawa Simba

NA WINFRIDA MTOI

KATI ya wachezaji vipenzi vya mashabiki wa kikosi cha Simba ni beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kiwango cha Tshabalala katika siku ya hivi karibuni, kimekuwa kikipanda, msimu akifanikiwa kumweka benchi Mghana, Asante Kwasi.

Licha ya kuletewa wapinzani katika nafasi anayocheza, Tshabalala, ameendelea kutamba katika kikosi cha kwanza kwa sasa akiwa nahodha msaidizi wa timu.

Baada ya Kwasi kuondoka, msimu huu Wekundu wa Msimbazi hao, walimsajili Gadiel Michael, kuongeza nguvu katika eneo hilo la ulinzi na kuleta ushindani zaidi.

Hata katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wamekuwa wakiitwa mabeki wote wawili, hali inayomfanya kila mmoja kupambana ili kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Kiufundi wachezaji hao kila mmoja ana vitu vyake vinavyoweza kumshawishi kocha kumuanzisha kikosi cha kwanza kulingana na aina ya mchezo wanaokutana nao.

Ukiangalia katika mechi nne za ligi kuu Simba walizocheza na kukusanya pointi zote 12, Tshabalala ameanza zote, hali inayoonyesha bado nyota huyo anamkimbiza.

 Kutokana na hali hiyo,kitendo cha Gadiel kuingia katika tuhuma za utovu wa nidhamu, kinampa nafasi zaidi Tshabalala ya kuaminiwa na benchi la ufundi.

Gadiel ambaye amesajiliwa na Simba kutoka Yanga, huenda sakata hilo likamuweka pabaya zaidi, hasa kwa wapenzi wa timu hiyo ambao wanaendelea kumuamini Tshabalala kuliko yeye.

Kutokana na utamaduni wa mashabiki wa timu za Simba na Yanga, inakuwa ni ngumu kumkubali mchezaji kirahisi hadi pale atakapofanya vitu vinavyowavutia.

Tshabalala tayari ameshaziteka akili za wapenzi wa timu hiyo, kazi kubwa ipo kwa Gadiel, lakini kutokana na tuhuma hizo za utovu wa nidhamu kwa kushindwa kwenda katika mechi muhumu, itamharibia.

Licha ya usajili wake kuwa wa kishindo kwa sababu alitokea Yanga, lakini alihitaji kujiweka vizuri kinidhamu na kuhakikisha anazivuta hisia za wapenzi wa timu hiyo, huku akiimarisha zaidi kiwango chake.

Gadiel na wachezaji wengine wa kikosi hicho, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Clatous Chama, wanatarajia kufikishwa katika Kamati ya Nidhamu ya Klabu ya Simba baada ya kushindwa kuungana na wenzao katika mechi za Kanda ya Ziwa.

Wachezaji hao hawakuwapo katika kikosi kilichovaana na Kagera Sugar, wakishinda 3-0 kwenye Uwanja Kaitaba, Bukoba na Biashara United walioichapa 2-0, Dimba la Karume, Mara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*