Tizi la Morrison acha kabisa

NA MWAMVITA MTANDA

ILI kujilinda zaidi na maambukizi ya virus vya ugonjwa wa Corona, nyota wa Yanga, Bernard Morrison, anapiga tizi la hatari nyumbani kwake ili pia kuendelea kulinda kiwango chake.

Akizungumza na BINGWA jana, Morrison alisema anafanya mazoezi ya nguvu kila siku asubuhi na jioni, zaidi akikimbia kusaka pumzisha na mengineyo ya kumjenga tayari kukinukisha shughuli za michezo zitakaporuhusiwa baada ya kusimamishwa kutokana na hofu ya kuenea kwa virus vya Corona.

“Najua nitakuwa na kibarua kizito tutakaporudi kazini, hivyo najipanga kwa mazoezi, sina muda wa kulala wala kupoteza, lazima nipambane kujiweka fiti kiwa ajili ya timu yangu,” alisema Morrison.

Mchezaji huyo alisema ana matumaini makubwa juu ya timu yake na kwamba hata kama inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiamini wanaweza kumaliza hata nafasi ya pili.

“Kazi ipo kwetu, tunapaswa kupambana, tusikate tamaa na muda wa kujitafakari ndio huu, kila mmoja ajiulize wapi anakosea ili tukirudi, kazi iwe moja,” aliongeza Morrison.

Morrison ametokea kuwa kipenzi cha Wanayanga kutokana na kandanda lake maridadi ndani ya timu hiyo, lakini akiwakuna zaidi Wanajangwani hao kwa bao lake aliloifunga Simba Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao hilo liliiwezesha Yanga kutoka uwanjani na ushindi wa 1-0 dhidi ya watani wao hao wa jadi, huku Morrison akiwa ndiye shujaa wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*