Tajiri wa masikini- 76

Ilipoishia

 “Samahani kwa kosa langu najua unafahamu nilifanya vile kwa sababu gani Vanuell. Najua unatambua fika jinsi gani moyo wangu unavyopata tabu juu yako.”

 “Hayo yalishapita Lucy yafaa tutazame yajayo,” nilimwambia.

 “Nashukuru kwa kunisamehe na kumfanya Theresa anisamehe pia, lakini pamoja na yote hayo bado naumia sana juu yako na sijui nifanye nini?”

SASA ENDELEA…

“HUNA la kufanya Lucy kwa sababu furaha ya Theresa iko kwangu nami pia furaha yangu iko kwake,” niliongea.

 “Vanuell kumbuka uliniahidi kuwa nikiacha pombe na sigara nitakuwa wako daima nami nimefanya hivyo nimeweza kazi hiyo ngumu.”

 “Nakupa pongezi kwa kufanya hivyo, hiyo ni faida ya mwili wako pia Lucy lakini nasikitika kukwambia siwezi kuwa nawe nahitaji kumlinda Theresa.”

Niliposema hayo nilipanda ngazi na kumuacha pale nje akitokwa na machozi, hata mimi moyo wangu uliniuma sana kwani siku zote sikupenda kumuumiza mwanamke yeyote yule kimapenzi. Niliingia ndani ya hekalu la tajiri Alenxender na kupanda ngazi moja kwa moja kuelekea sebule ya juu. Nilipofika huko nilimkuta Theresa akiwa na baba yake wakizungumza mambo yao, Theresa aliponiona alinikimbilia kama kichaa na kunikumbatia, nami nilimlaki kwa woga huku macho yangu yakigongana na ya baba yake aliyekuwa akinitazama kwa hasira ya mbali.

 “Karibu mpenzi karibu sana,” aliongea Theresa kwa uchangamfu mkubwa huku akinishika mkono.

Alinileta hadi kwenye kiti na kunikaribisha, kisha akakaa pembeni yangu, tajiri Alexender alizidi kunikazia macho tu. Muda mfupi baadaye watumishi watatu wa nyumba hiyo walileta vinywaji mezani. Kama kichaa Theresa aliongeza msumari wa uhasama kati yangu na baba yake kwa kusema.

 “Baba naomba nitoe shukrani zangu kwako, kwa kuniruhusu niwe na Vanuell. Nilishindwa kuamini kama umenipa furaha hii, najua ulitambua kuwa furaha yangu ni kuolewa naye, furaha yangu ni kuketi pamoja naye bustanini.”

Aliposema hivyo alimfuata baba yake na kujilaza kwenye kifua chake.

 “Asante baba kwa kujali hisia zangu na kunipenda kiasi hicho. Nampenda Vanuell kuliko kijana yeyote hapa chini ya jua, nashukuru umetambua bila yeye hakika nitakufa,” aliongea.

Mimi niligundua kuwa maneno hayo yalikuwa mwiba masikioni mwa tajiri Alexender aliyekuwa akinikazia macho akionyesha kukasirishwa sana. Lakini mwanaye alipomtazama usoni alijifanya kutabasamu, akijilazimisha kumuonyesha mwanaye kuwa alikuwa akiyafurahia maneno yake. Baadaye alisema.

 “Naomba utupishe nataka kuzungumza na Vanuell.”

Theresa alinitazama mimi na kisha akamtazama baba yake, nilihisi kuwa alikuwa amegundua kuwa kulikuwa na tatizo. Lakini alitabasamu na kuondoka mbele yetu ambapo alielekea chumbani kwake. Tajiri alinigeukia mimi akinitazama kwa macho ya hasira huku moyo wangu ukienda mbio nikiogopa sana.

 “Ewe mtunza bustani naona badala ya kufanya kile nilichokuagiza ndio kwanza unaharibu,” aliongea.

Nilibaki kimya huku nikitetemeka kwa mbali.

 “Nilikwambia umpe furaha mtoto wangu lakini si furaha hii bandia. Hivi anajua ni jinsi gani baba yake ninavyoyachukia mapenzi yenu, inamaana kazi yangu umeshindwa kuifanya? Unazidi kumfanya mwanangu kuwa mjinga mbele yako ewe fukara wa Adorra,” aliongea kwa hasira kuu.

Kwa woga na mwili wa kutetemeka nilimwambia.

 “Mkuu hakuna furaha itakayoufurahisha moyo wa binti yako zaidi ya hii.  Unadhani siku ile ningemwambia kuwa baba yako amekataa mimi kuwa nawe nini kingetokea, ukizingatia alikuwa ametoaka kuamka? Niliona nafasi pekee ya kuendeleza  furaha yake ni kumwambia uongo huo.”

 “Sitaki kusikia upuuzi huo ewe mtunza bustani, ninachotaka mimi ni wewe kufanya juhudi zote kukatisha mapenzi kati yako na binti yangu, nataka umuache kama ulivyomkuta mara ya kwanza. Hivi unadhani mimi tajiri wa kwanza barani Afrika naweza kukuruhusu mtu kama wewe tena Mpache umuoe binti yangu hivi nitakuwa na akiki kweli?”

 “Mkuu najua unaumia jinsi gani kuona mwanao anafuraha juu ya pendo lake kwangu, lakini sio mimi ninayeweza kumzuia ingawa ukweli najitahidi kutafuta furaha ya urafiki. Nipe muda nitakuwa nimelifanikisha hili mzee wangu,” niliongea kwa huruma zote.

 “Sikiliza ewe Mpache nakupa muda wa mwezi mmoja uwe umemtoa mwanangu katika utumwa huo. Mwanangu hakuwaga hivi, siku zote alikuwa hawapendi vijana wa kiume hakuona mwanaume yeyote wa kumpa furaha ya kimapenzi, iweje wewe masikini unayetoka katika vitongoji vichafu upendwe naye. Kwanza muda mwingine nahisi kuwa kuna dawa za uchawi utakuwa umempa.”

 “Hapana usiseme hivyo mkuu wangu, mapenzi huota sehemu yoyote ile.”

 “Hakuna kitu kama hicho, mwanangu alimkataa kijana kutoka Ujerumani tajiri wa kwanza kijana wa Bara la Ulaya, iweje akukubali wewe. Sina maneno mengi tena ewe mtunza bustani, usipofanya nayotaka hakika nitakuondoa katika uso wa dunia.”

Aliposema hayo, haraka alibadilisha sura ya hasira na kuifanya ya furaha ya uongo, kwani Theresa alikuwa anakuja pale sebuleni.

 “Bila shaka mmemaliza baba nataka kwenda naye bustanini,” aliongea Theresa kwa tabasamu zuri sana.

 “Ni ruhusa kwako kwenda naye tumeshazungumza mambo mengi na tumaini atakuwa amenielewa,” aliongea tajiri Alexender huku akinitazama mimi kwa macho yanayonihukumu.

Niliinuka kwenye kiti na kukiinamisha kichwa changu chini mbele yake, Theresa akiwa amenishika mkono huku akiwa ubavuni kwangu. Tuliondoka pamoja naye tukimwacha tajiri Alexender pale sebuleni. Moja kwa moja tulielekea bustanini wakati tukipita kuelekea huko, nilimwona Lucy akitutazama kupitia dirishani katika ofisi yake.

Tuliingia bustanini tukitembea taratibu, ndege kama mbuni, framingo, tausi na Ragbird walikuwa wakitufuata nyuma huku vipepeo wanaompenda Theresa nao wakiongezeka na kutua kwenye miili yetu. Tulipofika kwenye kiti chake, alinitazama sana na kisha akaniuliza.

 “Kuna tatizo mpenzi?”

Nilijilazimisha kutabasamu na kuyatazama macho yake na kumjibu.

 “Hakuna tatizo malaika wangu.”

 “Sio kweli Vanuell, niambie kuna jambo gani baya au nimekuudhi?”

 “Hujaniudhi Theresa wangu.”

 “Kama hakuna tatizo iko wapi ile furaha yako?”

 “Sina furaha kwa sababu naogopa sana kuwa na wewe.”

 “Kwanini uogope?” aliuliza kwa mshangao.

 “Siamini kama nitakuwa na furaha endapo nitakuoa wewe, kwa sababu wewe ni msichana mzuri unayependwa na kila mwanaume, kila mtu atanitazama kwa macho ya hasira pia sidhani kama nitaweza kukutunza.”

Theresa alitabasamu akanitazama kwa macho ya huruma na kunishika kichwani.

 “Vanuell nisikilize mpenzi, Mungu amenipa wewe kama bahati ninayotakiwa kuipokea na kutoiachilia. Sitaki mtu yeyote yule, wewe kuwa masikini ndiko kunanipa mimi furaha ya kweli. Usiogope wanaume wengine wanaonitamani na kunihitaji, jambo jema ni kuwa baba yangu kakuruhusu unioe hilo ndilo jambo muhimu zaidi. Hata ukisema tukaishi Adorra au Katanga mimi nitabeba kila kitu na nitakuja.”

Yalikuwa ni maneno mazuri sana kama vile yalitoka kwa malaika wa mbinguni, yalinifanya nijihisi paradiso. Lakini hata hivyo maneno ya baba yake yalizidi kusikika masikioni mwangu. Niliogopa kuendeleza kiburi changu cha kumfanya Theresa anipende kwani nilikuwa nina familia inayonitegemea pamoja na watu wa Adorra na Katanga.

 “Nashukuru kwa maneno yako mazuri malaika wangu,” nilimwambia.

Alitabasamu akanishika tena mkono, kwa mara ya kwanza alianza kunisogelea karibu kabisa na uso wangu, aliyafumba macho yake taratibu huku akiuleta mdomo wake laini katika mdomo wangu, nilishikwa na woga huku nikitetemeka sana. Nami niliyafumba macho yangu taratibu, huku nikianza kuhisi upepo wa pumzi yake ukinijia na kunipa hisia kali, hisia ambazo sikuwahi kuzipata tangu nilipozaliwa.

Nikiwa katika hali ya kufumba macho, nilishtuka baada ya mdomo wake kuuguza mdomo wangu, hatimaye alinibusu. Nami nilitamani aendelee kufanya hivyo siku zote za kuishi kwangu ingawa niliogopa sana.

Alipofanya hivyo, alirudi nyuma nilikuja kushtuka baadaye na kumuona akinitazama kumbe yeye alishakuwa amefumbua macho saa nyingi, akiniacha mimi nimeganda kama sanamu nikilitafakari busu lake tukufu. Nilijipoteza kwa kujizindua haraka na kumwabia.

 “Asante kwa zawadi yako.”

 “Asante kwa kushukuru,” aliongea akitabasamu.

Baadaye nilimwambia kuhusu ule mpango wa vitongoji vyetu kujitoa katika serikali kuu. Nilimwabia kuwa tayari watu wa Adorra na Katanga walishakuwa wameanza maandamano. Lakini yeye aliniambia.

 “Mpenzi unajua nilikuwa nakusubiria wewe ili nikuage,” aliniambia.

 “Unataka kwenda wapi tena,” nilimuuliza kwa mshangao.

 “Si ni juu ya jambo hilo nataka kwenda Ujerumani, kwenda kukamilisha suala lenu.”

 “Ohooo asante sana malaika wangu.”

 “Lakini niligundua kuwa ni vema tukaenda pamoja.”

 “Tukaenda pamoja?”

 “Ndio mpenzi.”

 “Hapana hiyo ni ngumu nitapata usumbufu wa kupata hati ya kusafiria, mimi ni Mpache mpenzi.”

 “Nafahamu Vanuell lakini ni lazima twende wote hadi Berlin kwa sababu lazima watataka wakuone wewe unayewaongoza watu wako katika hitaji lenu.”

Theresa alinitaka kwenda naye Ujerumani ili kufikisha hitaji hilo katika koloni hilo la zamani la nchi yetu. Aliniambia kuwa ni muhimu mimi mwenyewe kuwepo ili kutia sahihi karatasi za vitongoji vyetu za kujitoa katika serikali kuu ya Canibella.

Aliniambia yeye atakuwa mwongozo wangu, akisema atanisaidia kupanda ndege kuelekea huko. Sikuwa na budi kukubaliana na jambo hilo ambalo sikulitegemea, nilikubali kuelekea pamoja naye Ujerumani.

*********

Wakati mimi nikielekea Adorra, yeye alikwenda idara ya usafiri wa anga kwenda kutafuta hati yangu ya kusafiri.  Nilirudi Adorra na kukutana tena na maelfu ya wakazi na kuendelea kuwaeleza umuhimu wa sisi kujitoa.

Nikiwa mkutanoni, walikuja askari na kunikamata ambapo walinipeleka kituo cha polisi cha Adorra kati, hasira za wananchi zililipuka zaidi, wote walikuja kukusanyika nje ya kituo cha polisi.

Nini kitaendelea? Usikose kesho 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*