Ndemla awagawa viongozi wa matawi Yanga

NA ZAINAB IDDY

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba, Said Ndemla, amewagawa wanachama na viongozi wa matawi ya Yanga baada ya kuwapo kwa tetesi anajiunga na klabu hiyo.

Ndemla ambaye ni kipenzi kikubwa cha mashabiki wengi  wa soka nchini, hasa kutokana na uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali, anatajwa kuwaniwa na Yanga kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania  Bara.

Wakizungumza na BINGWA nyakati tofauti, baadhi ya  wanachama wa Yanga walisema ni faida kwao kumpata kiungo huyo huku wengine wakipinga kutua katika klabu hiyo.

“Binafsi siafiki kabisa Ndemla kusajiliwa Yanga, huyu ni mamluki anakuja kwetu ili kuiba mbinu na aondokea kama alivyofanya Ibrahim Ajib.

“Kwa kweli kumleta huyu Yanga ni bora hata wapewe mikataba Awesu Awesu, Salum Kihimbwa au Ismail yule wa Tanzania Prisons sio huyu bwana, kwanza ni wa kawaida tu ndio maana yupo tu pale Simba,” alisema

Amosi Zacharia mwanachama kutoka tawi la Yanga Ubungo Terminal

Kwa upande wake, Katibu wa matawi Mkoa wa Morogoro, Edward Mhagama, alisema wakimpata Ndemla atakuwa na faida kubwa Jangwani kutokana na ubora wake.

“Ndemla si mchezaji mbaya hata kidogo ni kakosa tu kuaminiwa kama yupo katika ripoti ya kocha, viongozi wafanye hima kumsajili kwa sababu anaonekana ana kitu anacho cha kuja kuipa Yanga,” alisema.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Mhezi,  alisema wakifanikiwa kumsajili Ndemla itakuwa ni faraja kwa wanaYanga.

“Ndemla anaweza kutupa faraja kama ilivyokuwa kwa Kelvin Yondan, wengi wetu tunajua tulimsajili akitokea Simba, hata Ndemla ni vizuri lakini iwapo kama kocha atamhitaji,” alisema Mhezi.

Hata hivyo,  Mhezi alisema Ndemla asije kwetu ili kuwakomoa Simba au kuwafurahisha watu fulani ndani ya Yanga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*