googleAds

Nchimbi: Kucheza na Molinga raha

NA ZAINAB IDDY

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Ditram Nchimbi, amemtaja David Molinga kuwa ndiye anayempa raha kila wanapocheza pamoja, ikiwa ni baada ya kutengeneza pacha hatari hivi karibuni.

Tangu aliposajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili mwezi uliopita, Nchimbi ameonekana kuelewana vilivyo na straika Mkongo, Molinga, wakiisaidia timu yao hiyo kuendelea kukusanya pointi msimu huu.

Kombinesheni hatari ya wawili hao ilianza kuonekana katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Ruvu Shooting, Nchimbi akitoa asisti tamu kwa Molinga, pia, alikuja kufanya hivyo tena Wanajangwani walipomenyana na Mtibwa Sugar.

Akizungumza na BINGWA jana, Nchimbi alisema baada ya kucheza michezo michache sambamba na Molinga ameanza kuielewa mikimbio ya mshambuliaji mwenzake huyo na jinsi gani ya kumpenyezea pasi za kufunga mabao.

“Nafurahi mno ninapocheza na Molinga. Sasa nafahamu ni aina gani ya pasi za kumpenyezea na katika mazingira yapi ili aweze kufunga mabao.

“Uzuri ni kwamba Molinga ana uelewa mkubwa wa mchezo wa soka, hata kama hana kasi, lakini anajua aina ya pasi ninazomletea njiani kutokana na mimi pia nimeshafahamu nimchezeshe vipi,” alisema.

Tangu ajiunge na Yanga, Nchimbi bado hajafanikiwa kuifungia bao, lakini uwezo wake wa kukaba na kukokota mpira unaonekana kuwa na faida ndani ya timu hiyo kupitia kwa wachezaji wenzake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*