googleAds

MTOTO WA LWANDAMINA AWAFUMBUA MACHO YANGA

NA HUSSEIN OMAR

JUNIOR Lwandamina ambaye ni mtoto wa Kocha Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina, amewafungukia wachezaji wa timu hiyo kwa kuwataka kuweka pembeni masilahi binafsi na badala yake kujituma uwanjani kama wanataka kufika mbali.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya wachezaji Yanga kugoma wakidai kutolipwa fedha zao za mishahara ya Novemba, siku mbili kabla ya kucheza na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Matokeo yake katika mchezo wao huo uliopigwa Ijumaa ya wiki iliyopita, Yanga ililazimisha sare ya bao 1-1 na African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam hivyo kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kuwajia juu wachezaji wao kwa kuwaambia matokeo yale yalikuwa ni matunda ya mgomo walioufanya.

Kauli ya Lwandamina Junior anayecheza katika klabu ya Young Buffaloes inayoshiriki Ligi Kuu nchini Zambia, haina tofauti na ile iliyotolewa na mashabiki wa Yanga baada ya mechi hiyo ya Ijumaa.

Akizungumza na BINGWA jana, Junior alisema baba yake anachukizwa na wachezaji ambao hawachezi kitimu na wanaoendekeza ubinafsi na kuweka mbele masilahi binafsi kuliko kazi.

“Naijua Yanga, ni timu kubwa, baba yangu katika maisha yake ya soka, hapendi wachezaji ambao hawachezi kitimu na ambao wanapenda kuweka masilahi yao mbele,” alisema Junior.

Aliongeza kuwa mzazi wake huyo, anapenda kufundisha timu ambayo itampa mafanikio pia ni mtu ambaye hapendi kuona mambo ya ubabaishaji katika suala zima la uendeshaji wa timu, hasa katika mambo ya utawala.

“Kwanza baba yangu hapendi siasa kabisa katika mambo ya soka, usije kushangaa anakaa muda mfupi halafu akaondoka huko Tanzania, anapenda kwenda kitaalamu zaidi,” aliongeza Junior.

Alisema Yanga ni timu kubwa katika ukanda wa Afrika na Wazambia wengi nchini humo wameanza kuisapoti na kuifuatilia mwenendo wake katika Ligi Kuu Bara baada ya baba yake kutua kukinoa kikosi hicho cha Jangwani.

“Ujue Yanga ni tofauti na Zesco. Huwezi kulinganisha Zesco na Yanga hata kidogo. Pia mazingira ya kufanyia kazi huko kwenu Tanzania ni mazuri, watu wanapenda sana soka tofauti na huku kwetu,” alisisitiza.

Alisema mashabiki wa soka nchini Zambia wamekuwa wakisoma taarifa za Yanga kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, hivyo wanaposikia habari mbaya, huumia mno wakijua zinaweza kumwathiri Mzambia mwenzao huyo katika kazi yake.

“Baba huku amekuwa maarufu sana tena mara mbili zaidi kuliko wakati anaifundisha Zesco. Kwa sababu kila kukicha tunapata habari mbalimbali kuhusiana na Yanga,” alisema.

Lwandamina aliyeiongoza Zesco ya Zambia kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, amesaini mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi cha Yanga ambapo kwa sasa anapigania taji lake la kwanza la Ligi Kuu Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*