Kipenzi cha Ndayiragije huyoo Yanga

NA MICHAEL MAURUS

YANGA ipo katika mkakati mzito wa kumsajili kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kupiga pasi za rula, lakini pia akiwa ni fundi wa mtindo maarufu ndani ya klabu hiyo wa kampa kampa tena, Vovatus Dismas.

Dismas, kiungo mkabaji mwenye umri wa miaka 18, kwa sasa anakipiga katika kikosi cha Biashara United ya mkoani Mara, wapenzi wa soka nchini wakimkumbuka kutokana na bao lake la hivi karibuni katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliopigwa Februari 22, mwaka huu, Dismas aliunasa mpira na kuuachia fasta kwa mchezaji mwenzake wa Biashara aliyempasia Atupele Green ambaye naye alimmegea pande maridadi kiungo huyo anayetakiwa Yanga ambaye alimchungulia kipa wa Simba, Aishi Manula na kuujaza mpira kimiani kwa guu lake la kushoto.

Bao hilo ndilo lililotibua rekodi ya Manula ya kucheza mechi tatu bila kuruhusu bao (clean sheet), japo halikutosha kuinusuru Biashara kupokea kipigo cha mabao 3-1.

Na sasa Yanga wameamua kumfungia kazi kiungo huyo fundi wa kupiga mapande ya maana, zikiwamo pasi ndefu zinazomfikia mlengwa kama alivyokuwa akifanya kiungo mahiri aliyewahi kutamba Jangwani na Simba, Athuman Idd ‘Chuji’.

Yanga wanamwona Dismas kama chaguo sahihi katika kuimarisha safu yao ya kiungo, hasa kwa wakati huu ambao wapo katika hatihati ya kumpoteza Papy Tshishimbi anayetajwa kuwa njiani kutua Msimbazi.

Watu wanaoujua mpira ndani ya Yanga, wameushauri ungozi wa klabu hiyo kufanya kila wawezalo ili kumsajili Dismas ambaye kwa bahati nzuri, hata kocha wa Wanajangwani hao, Luc Eymael amekiri kuvutiwa na kiwango chake.

Akizungumza na BINGWA jana kutoka nchini kwao Ubelgiji, Eymael alisema japo Dismas hakuwa katika mipango yake, lakini anamfahamu vema, akikiri ni miongoni mwa viungo bora Ligi Kuu Bara.

“Ni kiungo mzuri, japo hakuwa katika mipango yangu, lakini naweza kumfikiria na kuona kama tunaweza kumpata,” alisema Eymael ambaye aliwahi kuliambia BINGWA kuwa kikosi chake cha msimu ujao kitakuwa bab kubwa.

Ukiachana na Eymael, hata Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla ambaye naye ni mtu wa mpira, akiwa amelitumikia soka la Tanzania kama kocha kwa ngazi ya klabu na timu ya Taifa, Taifa Stars, alikiri kuvutiwa na Dismas.

“Ni mchezaji mzuri, nimeshawahi kumuona mara kadhaa,” alisema Dk. Msolla japo alipoulizwa na BINGWA kama yupo katika mpango wao, hakukubali wala kukataa zaidi ya kusema watamsikiliza kocha wao, Eymael iwapo atamuhitaji au la.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia BINGWA jana kuwa japo Dismas hakuwapo katika hesabu zao, lakini baada ya kumfuatilia kwa kina juu ya uwezo wake, wameona kuna umuhimu wa kumsajili ili kukabiliana na pengo linaloweza kuachwa na Tshishimbi iwapo hataongeza mkataba Jangwani.

“Ukweli ni kwamba Tshishimbi kuna uwezekano wa kumpoteza na inaonekana kuna sehemu ameahidiwa dau nono na sisi hatuwezi kumbembeleza maana inaonekana anataka kutukomoa kwa kututajia dau kubwa. Ni kweli ni mchezaji mzuri, lakini wakati mwingine huwa anazingua sana.

“Sasa katika kuchungulia huku na huko, tumepewa jina la huyo dogo wa Biashara (Dismas) na watu wengi wanamkubali, tunawasiliana na mwalimu kujua msimamo wake kwani yeye ndiye bosi wa benchi la ufundi hivyo tusingependa kumwingilia katika majukumu yake. Hata Tshishimbi akiondoka, tukimpata huyu, hakuna shida,” alisema bosi huyo ambaye hakupenda jina lake kuwekwa wazi.

Siku Biashara United ilipocheza na Simba Uwanja wa Taifa, Februari 22, mwaka huu, BINGWA lilipata fursa ya kuzungumza na kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije ili kupata maoni yake kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na Dismas katika kipute kile.

“Novatus ni mchezaji mzuri sana, namfahamu muda mrefu tangu akiwa Azam na ninamkubali sana, anajua mpira, atakuwa ni tegemeo la timu ya Taifa kwa siku za usoni,” alisema Ndayiragije aliyejizolea sifa kede kede kutokana na mafanikio yake ndani ya Taifa Stars.    

Wachambuzi kadha wa kadha wa soka nchini, wamekuwa wakimtaja Dismas kama kiungo wa kisasa mwenye kila sifa ya kupewa ‘dimba la chini’.

Miongoni mwa wachambuzi hao, yupo George Ambangile wa Wasafi FM ambaye hivi karibuni alimjumuisha Dismas katika kikosi chake bora kabisa cha msimu huu hadi ligi iliposimama, akimpiku Jonas Mkude wa Simba, lakini pia Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga na viungo wengineo wakabaji.

Akimwelezea kiungo huyo, Ambangile aliandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter akisema: “Novatus Dismas; Huyu ndiye kiungo mkabaji (Defensive Midfielder) aliyenivutia sana katika Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka klabu ya Biashara.”

Wadadisi wa mambo ya soka nchini wanaamini Yanga itakuwa sehemu sahihi zaidi kwa Dismas iwapo ataamua kuondoka Biashara United kwani ana uwezo wa kupata nafasi ya kucheza ndani ya Wanajangwani hao kuliko Simba kulikosheheni mafundi watupu kama Mkude, Clatous Chama, Mzmair Yassin, Said Ndemla, Sharaf Shiboub, Francis Kahata na wengineo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*