Kahata afanya mambo Kenya

NA MWANDISHI WETU, KENYA

KIUNGO wa Simba, Francis Kahata, amefanya mambo makubwa nchini kwao Kenya, baada ya jana kutoa msaada wa maji kwa ajili ya kujikinga na virus vya ugonjwa wa Corona.

Nyota huyo wa kimataifa wa Kenya, yupo nchini kwao huko kwa kipindi hiki ambacho shughuli mbalimbali zinazohusu mikusanyiko, ikiwamo michezo, zikiwa zimesimamishwa kuepusha maambukizi ya virus vya ugonjwa huo hatari unaoitikisa Dunia kwa sasa.

Katika msaada wake huo, Kahata ametoa maji lita 10,000 katika eneo la Mathare 4B, lililopo jijini Nairobi.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Kahata alisema mashabiki wake wa eneo hilo, walimuomba awasaidie maji hayo kwani hawakuwa nayo ya kutosha na hivyo nyota huyo kufanya hivyo.

“Mimi na rafiki zangu tumeamua kuwaletea maji hawa jamaa zetu ili kuwasaidia kujikinga na virus vya Corona,” alisema Kahata na kuongeza:

“Watu wamekosa hata maji ya kuoga na nimeamua kuwasaidia kwa kuwapa lita 10,000 na tumewaonyesha watoto jinsi ya kuosha mikono yao.

“Nadhani ni vema kuonyesha mapenzi yetu kwa watu kama hawa katika kipindi hiki kuliko kukaa tu majumbani.”

Msaada huo wa Kahata, umekuja siku moja baada ya nyota wa Harambee Stars na Montreal Impact, Victor Wanyama, kutoa msaada wa dawa ya kusafishia mikono (sanitizers) kwa wakazi wa Mathare.

Nyota wengine waliotoa misaada nchini Kenya kusaidia jamii kukabiliana na virus vya Corona ni Johanna Omollo na Eric Ouma.

Kahata alitua Simba msimu wa 2019/20 akitokea Gor Mahia ya Kenya, akiwa ni mmoja wa wachezaji wenye nafasi kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi hao wenye nafasi kubwa ya kutetea taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*