Inter Milan wao na Lukaku hadi kieleweke, watuma ofa rasmi Man United

MANCHESTER, England

KAMA kuna anayedhani Inter Milan wanatania juu ya Romelu Lukaku, basi atakuwa amekosea. Iko hivi, mabingwa hao wa zamani wa Italia, wametuma ofa rasmi ya kutaka kumng’oa straika huyo ndani ya kikosi cha Manchester United.

Baada ya msimu uliopita kumalizika, Inter Milan walimtangaza Antonio Conte kuwa kocha wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Luciano Spalletti aliyetimuliwa.

Tangu Conte aingie Inter Milan, amekuwa mstari wa mbele kushinikiza usajili wa straika huyo wa Ubelgiji ambaye mambo yake yanamwendea tofauti ndani ya kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer.

Juzi, Mkurugenzi wa Michezo wa Inter Milan, Piero Ausilio, alikutana na viongozi wa Manchester United ambao wapo tayari kumuuza Lukaku kwa kiasi cha pauni milioni 75 (sh bil 215).

Baada ya kikao hicho kilichodumu kwa zaidi ya saa mbili, Ausilio alisema kuwa timu zote mbili zimekubaliana, kwa hiyo, wanasubiri kuona kipi kitatokea kwa wakati ujao juu ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26.

“Nafurahi kuona makubaliano yamefikiwa na timu zote mbili, tusubiri muda tuone kipi kitatokea, wachezaji wote ambao tunahitaji kuwasijili tulikubaliana na Conte, tunahitaji kumpa anachokitaka kama bajeti inaruhusu,” alisema.

Hata hivyo, inafahamika kuwa ombi kubwa la Inter Milan ni kumchukua Lukaku kwa mkopo wa miaka miwili, kisha kumsajili jumla, wakati Manchester United wakiwa tayari kumwachia straika huyo kwa kitita cha pauni milioni 75.

Lukaku anataka kuondoka ndani ya kikosi hicho baada ya Solskjaer kusema straika huyo atakuwa chaguo la pili, nyuma ya Marcus Rashford, wakati anaingia Desemba mwaka jana kuchukua mikoba ya Jose Mourinho.

Lukaku hakushiriki mazoezi ya United ya juzi, kiasi cha kuamini kwamba nyota huyo anajiandaa kuondoka, lakini jana aliungana na wenzake mazoezini kwenye Uwanja wa Klabu ya Perth Glory ambayo watacheza nayo leo mchezo wa kwanza wa kirafiki.

Juzi, Solskjaer alisema timu hiyo haina mpango wa kuuza mchezaji yoyote kwa sasa, lakini hali ambayo inaendelea ndani ya kikosi hicho, itakuwa rahisi kwa kocha huyo kumfungulia milango Lukaku.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*