googleAds

EYMAEL AMTAJA NIYONZIMA SARE YA PRISONS

NA ZAINAB IDDY

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael, amesema kukosekana kwa kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima ni sababu mojawapo ya kushindwa kuondoka na pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons.

Yanga waliambulia pointi moja baada ya kutoka sare ya kutofungana na Prisons katka mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Eymael alisema Niyonzima ni mchezaji mwenye akili ya mpira anayeweza kufanya lolote timu inapokuwa imezidiwa.

“Kama Niyonzima angekuwepo angeweza kufanya kitu  kubadili mchezo huenda tungepata ushindi, huyu ni mchezaji mwenye akili ya mpira na anayeweza kufanya lolote  kubadili mchezo, tumeshindwa kuwa naye leo (jana) kwa sababu anaumwa malaria.

“Kila mtu anajua kipaji alichojaliwa Niyonzima ni mchezaji wa kipekee niliyewahi kukutana naye amekuwa mhamasishaji mkubwa kwa wenzake katika kuitafutia matokeo Yanga, mara nyingi anapokuwepo nakuwa na uhakika wa kupata matokeo ya kufurahisha,” alisema Eymael.

Eymael alisema kukosekana kwa mshambuliaji wa timu hiyo,  Ditram Nchimbi anayetumia adhabu ya kadi tatu za njano ni sababu nyingine ya kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Kwa ujumla nawapongeza wachezaji kwa jitihada walizoonyesha , bahati haikuwa yetu kwa sababu tulipata penalty, lakini Morrisons (Bernard) alikosa, simlaumu sana katika hili ameonekana hata mwenyewe ameumizwa,” alisema.

Kocha huyo, alisema anakwenda kufanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mchezo huo ili waweze kupata ushindi.

Yanga  wanatarajiwa kucheza na Polisi Tanzania katika mchezo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, mkoani Kilimanjaro.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*