ZAIID: WEMA HANIJUI, AMETUMIA WIMBO WANGU KUONYESHA AFRIKA ILIVYOBARIKIWA

MOJA kati ya nyimbo chache za hip hop nchini zilizopata mafanikio makubwa mwaka jana ni Wowowo. Wimbo kutoka kwa rapa Zaiid wenye maudhui ambayo kila mmoja wetu anaweza kuyatafakari vile atakavyoona inafaa.

Jiachie na Staa Wako leo hii tumefanya mahojiano maalumu na rapa huyo memba wa zamani wa familia ya Tamaduni Music ili kufahamu mengi kuhusu muziki na maisha yake, karibu.

BINGWA: Kwa ambaye ameanza kukufahamu hivi karibuni Zaiid ni nani?

Zaiid: Jina halisi naitwa Abdullah Mnete, ni mkazi wa Dar es Salaam asiliami mia, nimekulia Mwenge. Muziki nilianza kupenda nikiwa sekondari, nilikuwa narap ila nilikuwa sijui ni nini.

Nilipata bahati ya mjomba wangu ambaye ni moja ya waasisi wa muziki Tanzania anaitwa Zavara au Chief Rhymson wa Kwanza Unit. Yeye alikuwa anaishi nchini Marekani aliporudi nikawa naishi naye, nikamwambia nafanya, alifurahi na akaanza kunifundisha na kunielekeza vitu vingi sana, nikaanza kuwa karibu na kina KBC, Samia X na wengine wa Kwanza Unit.

Mwaka 2013 nikafanya ‘Mixtape’ (Kanda Mseto) ya kwanza iliyokuwa inaitwa Kanda Mbovu sababu nilikuwa nimechukuwa biti za nje lakini nimerap Kiswahili. Ndani yake kulikuwa na muziki unaoitwa Who Dat ambao watu waliuelewa, nilitumia biti ya J Cole.

Mwaka 2015 nikawa nimetoa ‘MixTape’ nyingine inayoitwa Mwenge Kiwalani niliyofanya na mwanangu P The Mc, tulifanya maboresho ya miziki na kufanya kwa ubora mkubwa sana.

BINGWA: Wazo la kuandika wimbo Wowowo ulilitoa wapi?

Zaiid: Wazo la Wowowo ni msamiati ambao kaka zetu walikuwa wanautumia sana kuwasifia wadada waliojaaliwa. Nilikuwa nao na sikujua nitautumia wapi, siku moja tulikuwa tunasikiliza wimbo wa Rihanna ile ‘Walk Walk Walk’ ikawa ‘ina-sound’ kama Wowowo.

Nikasema ngoja nitumie mawazo ya kaka zetu wa zamani nifanye kisasa hivi, nikasema nifanye kwenye aina gani ya mdundo, nikasema ngoja nifanye kwenye hii hii midundo inayoonekana migumu kwa watu. Wowowo imetengenezwa zaidi ya mara tatu studio tofauti.

Binafsi nasema Wowowo ni ushairi bora ambao unafurahisha na unafloo nzuri kwa mtu anayesikiliza.

BINGWA: Mrejesho wa wimbo huo kwenye jamii umekufundisha chochote kwenye uandishi wa ngoma zako nyingine?

Zaiid: ‘Impact’ yake ni kubwa sana, sikutegemea kwa sababu hata wakati naitoa Wowowo, sikufikiria itakuwa ‘hit’, nilitoa sababu ilikuwa tayari ‘ime-mixiwa’ kwa sababu huko kwenye akiba yangu kuna nyimbo nyingi tu zenye ubunifu ambazo zilikuwa ‘hazija-mixiwa’ (changanywa).

Kilichonifunza ni kuwa kila kitu kinawezekana, hakuna kitu kinachoshindikana, watu wajiamini si tu kwenye sanaa bali kwenye vitu vingine vyovyote.

Wowowo ni wimbo niliofanya mimi, ‘production’ si ya watu maarufu sana na sijashirikisha mtu yeyote ila imekuwa ‘hit’ kwa hiyo mimi imenifunza kuwa mimi nina utunzi bora sana.

SWALI: Mpaka sasa umekupa mafanikio gani?

Zaiid: Wowowo ni ngoma iliyopiga hatua kuliko nyimbo zangu zote. Ni moja kati ya ‘track’ chache za hip hop Tanzania ambayo imevuka mipaka ya ‘hit’.

Hapa katikati ilikuwa ngumu nyimbo za hip hop kupenya bila kuathiri au kuwa na msukumo wa kitu chochote nyuma, lakini wimbo wangu umeingia vijijini, unapigwa kila sehemu ipo kwa vizazi vyovyote.

Imenifanya niwe mkubwa sana, nimepata dili za matangazo, nimezunguka sana kwenye shoo, nimefanya watu waniamini na umefungua milango mingi.

BINGWA: Umeipokeaje ile video ya Wema Sepetu akicheza Wowowo?

Zaiid: Kitu ambacho nimefurahi mapokeo ya wengi sana lakini Wema amenifurahisha zaidi kwa sababu kwa muda mrefu watu wamekuwa wakimsakama kuwa ‘Mchina’.

Kwa hiyo kama ametumia Wowowo kujibu hizo tuhuma ‘indirect’, mimi naona ni kitu kizuri kwa sababu mtu anatumia wimbo wangu kuwa fahari na umbo lake ni kitu sawa sana. Nimeimba Uafrika na nimefurahi sana madada zetu kama Wema kuonyesha kama sisi tumebarikiwa, ni sapoti.

Mimi sijawahi kukutana na Wema kwa hiyo hafanyi vile sababu ananijua, amefanya kwa sababu anauzimia muziki na watu wengine wawe ‘proud’ kama alivyofanya yeye.

BINGWA: Unauzungumziaje utaratibu wa kuzifungia nyimbo zisizo na maadili?

Zaiid: Nimejaribu kufuatilia japo sijafuatilia kwa asilimia mia, lakini kwa asilimia chache nilizofuatilia haya mambo ya kufungia miziki sijajua kwanini hasa na wanazingatia vitu gani.

Kwa sababu kwa mimi sanaa ni lugha ya picha ambayo ni tofauti na watu wanavyofikiria, kwa hiyo ukifungia muziki kwa sababu mimi nimesema ‘mke wangu anakula tango’ halafu mimi maana yangu anakula tango kama tango na wewe umefikiria vingine ukafungia muziki wewe utakuwa umekosea si mimi.

Kwa hiyo watu wanafungia muziki kwa tafsiri binafsi, hilo ni kosa kubwa kisanaa. Mimi nadhani haya mabaraza yaajiri wahusika wa sanaa kwa asilimia kubwa ili kupunguza hizo hali za mitafaruku sababu sanaa ina lugha pana sana.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*