googleAds

Azam yawatisha Yanga

NA ZAITUNI KIBWANA
KOCHA Mkuu wa Azam, Meja Mstaafu Abdul Mingange, amesema kikosi hicho kitaingia kambini Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga.


Azam FC itavaana na Yanga, Aprili 29, mwaka huu katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA jana mara baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka Mtwara, Mingange alisema atavaana na Yanga akiwa na kikosi kamili tofauti na alivyocheza na Ndanda FC.


“Tulicheza na Ndanda huku wachezaji wengi wakiwa majeruhi lakini tutakapoivaa Yanga kikosi kitakuwa kamili ili kuhakikisha tunaibuka na pointi tatu,” alisema Mingange.


Akizungumzia mchezo dhidi ya Ndanda, Mingange alisema wachezaji wake walichoka na safari ndio sababu ya kupoteza mchezo dhidi ya Ndanda FC, lakini sasa wamepata muda wa kupumzika na kujiandaa.
Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 66 baada ya kushuka dimbani mara 31, ikishinda 19, sare tisa na kupoteza tatu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*