Ajib amponza mwamuzi, kiungo Kagera Sugar

NA ZAINAB IDDY

KITENDO cha kiungo wa Kagera Sugar, Zawadi Mauya cha kumchezea mateke mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, kimemponza mwamuzi, Emmanuel Mwandembwa.

Mwandembwa alichezesha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliowakutanisha Kagera Sugar na Simba, Septemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba alishindwa kutoa adhabu stahili kwa Mauya.

Kutokana na kitendo hicho Bodi ya Uendeshaji wa Ligi (TPLB), imetoa onyo kali kwa mwamuzi Mwandembwa na kiungo huyo wa Kagera Sugar.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura, alisema baada ya kupitia mchezo huo, walibainia Mauya alistahili kupewa kadi nyekundu na si ya njano kama ambavyo ilitolewa.

“Video zilionyesha Mauya hakufanya kitendo cha uugwana kwa mchezaji wa Simba, kwani alimpiga mateke kwa zaidi ya mara tatu, hapa alistahili kadi nyekundu, lakini mwamuzi alimpa ya njano jambo linalomaanisha alishindwa kutafsiri vizuri sheria za mchezo wa soka.

“Kutokana na jambo hilo tumemuandikia barau ya onyo Mwandembwa kama atakuja kufanya kosa lingine katika mechi atakazopewa atakutana na adhabu ya kifungo, lakini pia tumetoa onyo kwa mchezaji wa Kagera kile alichokifanya hakikubaliki,” alisema.

Wambura aliongeza: “Katika kanuni za adhabu zipo za aina nyingi, hivyo tungeweza kutengua maamuzi ya mwamuzi, lakini kibusara na kulingana na tukio lilivyo tumetoa onyo kwa wote.”

Katika hatua nyingine, Bodi ya Ligi imetoza faini Shilingi milioni moja, timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC), baada ya kugoma kuingia vyumbani katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal United uliochezwa mjini Tanga.

Timu ya Alliance FC imetozwa faini shilingi milioni moja na nusu kutokana na mashabiki wao kufanya vurugu na kufanya vitendo vinavyoashirikia imani za ushiriki, adhabu ambayo imeikuta Biashara United. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*