Waamuzi tupeni bingwa wa ukweli FA

NA CLARA ALPHONCE

HII ni wiki ya mechi za Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC), hatua ya robo fainali, takribani timu nane zitakuwa viwanjani leo, kesho na keshokutwa kuwania kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Timu zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni Yanga, Singida United, Njombe Mji, Stand United, Azam FC, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.

Hii ni mara ya pili kwa michuano hiyo kufanyika, lakini kabla ilikuwapo na ilisimama kwa miaka kadhaa bila kufanyika.

Bingwa wa michuano hii ya Shirikisho ndiye ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kama ilivyofanya Simba mwaka huu.

Awali kabla ya kurudi kwa michuano hii, ilikuwa mshindi wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye anashiriki michuano hiyo, huku bingwa yeye akishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu uliopita bahati iliangukia kwa Simba, baada ya kumfunga Mbao FC 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Simba alikuwa hajashiriki michuano yoyote ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo, kutokana na kutofanya vizuri kwenye ligi, lakini akaibuka kwenye michuano hiyo ya FA msimu uliopita.

Hata hivyo, Simba imeshindwa kuendelea katika michuano hiyo baada ya kutolewa katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo na timu ya Al Masry ya Misri kwa jumla ya mabao 2-2, Waarabu hao wakiwa wamesonga mbele kwa faida ya mabao mawili waliyoyafunga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mpaka hapo umuhimu wa michuano hii ni mkubwa kwa soka letu Tanzania, hivyo ombi kubwa ni kwa waamuzi watakaochezesha hatua ya robo fainali kuhakikisha wanafuata kikamilifu sheria 17 za soka, ili tuweze kupata bingwa anayestahili bila kujali ukubwa wa timu.

Msimu uliopita kulikuwa na malalamiko mengi juu ya ushindi wa Simba, wengi wakilalamika kuwa, ilibebwa ili iweze kushiriki michuano ya kimataifa, baada ya kuikosa kwa muda mrefu.

Malalamiko kama hayo yanatia doa mashindano na soka letu kwa ujumla, mpira wa sasa unahitaji zaidi matokeo ya uwanjani na si mambo mengine.

Michuano ya kimataifa si lelemama, Simba na Yanga wanajua kwa kuwa wamekuwa wakishiriki mara kwa mara, lakini si kigezo cha kuwapa nafasi timu hizo kila mwaka kushiriki hata kama wameshindwa kupambana na kupata nafasi kwa nguvu zao.

Waamuzi imefika wakati wasaidie kuliokoa soka letu, kwa kuchezesha kihalali. Tunajua mwamuzi ni binadamu, hawezi kuwa sawa kwa kila kitu, lakini angalau asilimia 90 zitasaidia.

Hatuwezi kusema waamuzi wote wamekuwa wakifanya makosa kwa makusudi, wapo ambao wanashindwa kutafsiri sheria wawapo uwanjani na wengine wamekuwa wakifanya kwa makusudi kwa ajili ya zawadi aliyoahidiwa au kaamua tu kuwakomoa kwa sababu fulani.

Soka la Bongo limejaa dhuluma nyingi, siku zote bingwa hapatikani kihalali kutokana na magumashi mengi ambayo yamekuwa yakiharibu mpira, huku waamuzi wakichangia kwa kiasi kikubwa.

Pia timu zilizoingia katika michuano hiyo zipambane kupata matokeo, maandalizi mazuri ni moja ya sehemu ya matokeo mazuri, zionyeshe hazikuingia kimakosa katika hatua hiyo.

Msimu huu tunahitaji bingwa wa halali asiye na malalamiko ambaye atapewa baraka zote na klabu zote shiriki, kwenda kuwawakilisha katika michuano ya kimataifa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*