Mwanamke hapaswi kufanyiwa hivi kama unahitaji amani

NA RAMADHANI MASENGA

MWANAMKE ni binadamu kama mwanaume, anahitaji amani, furaha, kupewa thamani na kuheshimiwa kama anavyohitaji mwanaume.

Kosa kubwa wanalofanya wanaume wengi katika mahusiano ni kuwafanya wanawake wao kukosa uhuru na thamani.

Unakuta kama ni pesa ya matumizi, mume anampa mke kiwango kile kile anachopaswa bila kuzidisha kiwango chochote.

Wanawake wengi katika baadhi ya mahusiano wanaishi maisha yasio na tofauti na watoto wadogo kwa wazazi wao.

Kila kitu ni lazima waombe, kila jambo ni lazima wawasikilize wenzao wanataka nini, lakini wao hawana uhuru wa kusikilizwa ama kufanyiwa jambo wanalotamani kufanyiwa.

Wanaume wengi huona hali hii kama ya  kawaida ila ukweli ni kwamba ni hatari  inayoua upendo na hamasa ya wanawake kwa waume zao.

Mwanamke ni mshirika kwa mwanaume, kitendo cha mwanaume kuanzisha uhusiano naye wa kimapenzi maana yake anataka kumfanya mwanamke husika kuwa sehemu yake.

Sasa kama kweli ni sehemu yako, sehemu muhimu ya maisha yako, kwanini humpi hadhi inayostahili?

Wapo baadhi ya wanaume hawajulikani kwa wake zao wakiwa na pesa wala kipindi hawana, siku zote wao ni hali mbaya tu kwa wake zao, hii ni hatari mno.

Ifahamike, hakuna binadamu asiyependa kuishi vizuri ama kupata vizuri, sasa unavyomnyima fursa menzako kuonja ladha ya mafanikio ama chochote cha maana kutoka kwako, unamuumiza na kumfanya asione thamani yake kupitia wewe.

Mke wako anahitaji umiliki, awe na furaha na ajiachie kwa kuwa na wewe, hivyo unavyomfanya asijione sehemu muhimu ya maisha yako si tu unamnyima furaha, ila pia unaufanya uhusiano wako uwe dhaifu.

Kama mke wako haoni raha na amani kutokana na mtindo wa maisha yenu, unadhani hali hiyo ataendelea kuwa nayo mpaka lini?

Kama binadamu ni lazima atamani maisha ya kujiachia na kuiona thamani na hadhi yake stahili, hivyo kuwa makini, ukiacha kuziba ufa utajenga ukuta.

Mke wako ni zaidi ya rafiki, ni mshirika wako wa kihisia, mwili na maisha, mtu wa namna hii hapaswi wala kustahili kuonwa wa kawaida.

Mpe uhuru fulani katika matumizi na maisha yenu, mfanye ajione yuko kwake si yuko kwako.

Baadhi ya wanawake wanafanya mambo yasiyostahili katika maisha yao, mbali na mambo mengine ila tabia ya waume zao kuwaona ama kuwatendea kama watoto wadogo ni sababu nyingine.

Mwanaume anaenda kwenye matembezi na ‘pocket money’ ya kutosha ila mkewe anamuacha na pesa kamili ya matumizi muhimu.

Hata akitamani soda ama kitu kingine hawezi kununua, hii si sawa na haistahili kuwa hivi.

Kumnyima uhuru na hadhi anayostahili kunamfanya mwanamke husika ajione yupo kifungoni badala ya kuwa katika uhusiano.

Ndio maana tafiti zinaonesha katika ndoa nyingi wanawake hawana furaha bila sababu ya kueleweka.

Wanawake wengi hawana furaha na waume zao hawajui ni kwanini, hata wakati mwingine wanawake wenyewe wanasahau kwanini hawana furaha.

Ila ukichunguza kwa makini kwa jicho thabiti la kitaalamu, unagundua wengi wao hawana furaha katika mahusiano yao kutokana na namna wanavyofanywa kuishi.

Wakati baadhi ya wanawake wakiona waume zao wanafanikiwa hupata furaha isiyo kifani, wapo wengine ambao wanaona ni kawaida tu.

Hawana furaha kwa sababu wao huwa hawaoni tofauti kati ya waume zao wakiwa na fedha na kipindi wakiwa hawana.

Wao kila siku hali ni mbaya tu yaani wakati wote ni kuvumilia, wanaume inabidi kubadilika.

Toka na mkeo ‘outing’, mpatie pesa zisizo katika matumizi sahihi na mwambie atumie anachopenda yeye kutumia.

Mpe uhuru ili akuthamini zaidi, mthamini ili akujali na kukusikiliza zaidi, mapenzi ni urafiki wa ndani wa hisia, miili na fikra, mjali mwenzako aone hali hii kupitia matendo na kauli zako.

Katika maisha kila siku ni kupambana na changamoto, ila hali hii isikufanye umnyime mwenzako fursa ya kufurahi na kujidai na maisha yake.

Mwenzako anapaswa kusisimuliwa na matendo na kauli zako, namna unavyowatendea watoto wako haipaswi kuwa sawa na unavyomtendea mkeo.

Mkeo ni sehemu yako, kama ambavyo unavyopaswa kuheshimiwa, kujaliwa na kusikilizwa.

Mkeo pia anahitaji nafasi hiyo maana naye ni binadamu kamili kama wewe na si nusu yake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*