googleAds

ZULU ‘MKATA UMEME’ KAMA JAJA TU!

NA ONESMO KAPINGA

BILA shaka kichapo cha mabao 4-0 walichokipata Yanga kutoka kwa Azam FC katika mchezo wa makundi wa Kombe la Mapinduzi uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, kitakuwa kimewakasirisha mashabiki wao.

Ni kipigo kikubwa kwa timu kama  Yanga inayoundwa na nyota wengi wakiwamo wazawa na wageni wanajua kucheza mpira hasa ukizingatia walitoka kumpiga mtu mabao 6-0 katika michuano hiyo inayoendelea visiwani humo.

Hao walikuwa si wengine bali ni Jamhuri ya Pemba, waliopokea kichapo hicho, lakini baadaye Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto katika mfululizo wa mechi za michuano hiyo.

Lakini usiku wa juzi, naamini mashabiki wa Yanga hawakupata usingizi vizuri,  baada ya kupokea kipigo hicho huku  mastaa wao wote wakiwa ndani ya kikosi isipokuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Donald Ngoma na Obrey Chirwa.

Nadhani haikuwa siku nzuri kwa mashabiki wa Yanga kutokana na kipigo hicho ambacho wengi hawakutarajia kutokana na Azam kuanza vibaya kwenye michuano hiyo.

Pamoja na Azam kuonekana kusajili vizuri wachezaji, lakini tatizo lilikuwa katika benchi la ufundi ambalo hivi karibuni walitimua makocha wote kutokana na kufanya vibaya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pengine hiyo ilikuwa ni moja ya sababu ya Yanga kufungwa kwenye mechi hiyo, kwani waliiona Azam kama timu ambayo imepotea katika msimu huu, lakini ushindi walioupata mara mbili mfululizo inawezekana uliwapa kiburi.

Sikuwa na wasiwasi kama Yanga wangefungwa na Azam kutokana na kikosi chao kilichopangwa, kwani niliamini uwepo wa Kelvin Yondani na Andrew Vicent pale nyuma na pale kati Thaaban Kamusoko na Justine Zulu kama wengine wanavyomwita ‘Mkata Umeme’, nilijua shughuli ingekuwepo.

Mbele ya akina Kamusoko na Zulu kulikuwa na Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Amissi Tambwe na Juma Mahadhi, hakika jamaa walitimia kila idara na Azam wasingepata pa kutokea kabisa.

Lakini baada ya Azam kupata bao la kuongoza katika dakika ya kwanza ndipo nikaanza kufikiria katika dirisha dogo Yanga walifanya usajili wa namna gani?

Baadaye nilipata jibu kuwa walifanya usajili wa wachezaji wawili ambao ni mshambuliaji, Emmanuel Martin kutoka JKU ya Zanzibar na mwingine ni kiungo  mkabaji, Zulu kutoka klabu ya Zesco ya Zambia.

Kwa kuwa Yanga walikuwa na tatizo la kiungo mkabaji, nilitumia muda mwingi kujiridhisha na usajili wa Zulu ambaye aliletwa kwa shughuli ya kuunganisha  timu vizuri baada ya waliokuwepo kutoimudu vema nafasi hiyo.

Nilitumia dakika 45 za kwanza kufuatilia uwezo wa Mzambia huyo jinsi anavyoweza kumiliki mpira na kupandisha timu ili iweze kupeleka mashambulizi mbele, lakini  sikuona  kama atakuwa ni mtu wa msaada kwa asilimia 100.

Kiukweli Zulu hajaweza kunishawishi kama ni kiungo mkabaji mzuri  ambaye atakuja kuisaidia Yanga  hasa kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa itakayoanza mwezi ujao.

Mzambia huyo amenifanya nimkumbuke mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Mbrazil,  Genilson Santana Santos ‘Jaja’, aliyeletwa na aliyekuwa kocha mkuu wao, Marcio Maximo, ili kumaliza tatizo sugu la ukame wa mabao.

Maximo aliwaaminisha mashabiki wa Yanga kuwa Jaja alikuwa ni mshambuliaji sahihi, kwani baada ya muda mfupi angekuwa ni mtambo wa kutengeneza mabao pale Jangwani, lakini matokeo yake alikuja kuumbuka na kuamua kuikacha klabu hiyo, kwani alipokwenda kwao kwa mapumziko hakurejea tena nchini.

George Lwandamina ni kocha wa Yanga aliyetokea Zambia, amekuja na mchezaji wake, Zulu na kwa kuwa taaluma yake ni kufundisha mpira ametuaminisha kwamba Zulu ni kiungo mkabaji mzuri, lakini Mzee wa Kupasua anakataa.

Kwa dakika 59 alizocheza Zulu dhidi ya Azam bado hajaniaminisha uwezo wake  ukilinganisha na Martin waliosajiliwa pamoja katika dirisha dogo la Ligi Kuu Bara lililofungwa Desemba 15 mwaka jana.

Uwezo wa Zulu ni kama wa Jaja  aliyesajiliwa kwa  fedha nyingi, lakini mashabiki wa Yanga walikosa huduma yake nzuri, pale aliposhindwa kuwa mbadala sahihi  wa straika Mzambia, Davis Mwape.

Tukutane Jumatatu ijayo

kapssmo@gmail.com 0716985381


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*