googleAds

ZILIPENDWA

NA VALERY KIYUNGU


 

KARIBUNI  katika mwendelezo wa simulizi za mwanamuziki (marehemu) Marijani Rajabu. Wiki iliyopita niliishia kukumbushia baadhi ya maneno ya wimbo ‘Mwanameka’. Sasa endelea.

Marijani baada ya kutunga na kuimba wimbo ‘Mwanameka’, aliendelea kushiriki nyimbo kadhaa akiwa na bendi hiyo ya Dar International, huku baadhi ya mashabiki wake walimpa jina la ‘Kamusi inayotembea’, wakimfananisha na kitabu kinachoelezea maana ya maneno kinachoitwa kamusi.

Mkongwe huyo akiwa na nia ya kuwapa burudani mashabiki na wadau wa muziki wa dansi, alitumia muda wake mwingi na kipaji chake cha ubunifu, ambacho kilimwezesha kutunga nyimbo kila alipotaka kufanya hivyo.

Nyimbo kama ‘Mapambano Yanaendelea’, ‘Chakubanga’, ‘Mama Watoto’ na ‘Mashujaa’, ni miongoni mwa nyimbo ambazo zilimpa umaarufu, sambamba na bendi hiyo ya Dar International  kung’ara zaidi.

Kama wasemevyo Waswahili kuwa ‘kila masika na mbu wake,’ ikiwa na maana kwamba, kila wakati kunakuwa na tukio tofauti na lingine, kauli hiyo pia ilitumika katika matukio ya nyimbo za Marijani.

Nyimbo zake karibu zote alizokuwa akitunga zilikuwa  zinalenga matukio na visa katika jamii. Wimbo ‘Uzuri wa Asili’ ulikuwa ni miongoni mwa nyimbo zilizotungwa na kuimba mwaka 1978 na ulionekana kuwa ‘mwiba mkali’ kwa baadhi ya akina mama wa wakati huo.

Wimbo huo ulipewa majina mengi na mashabiki wa muziki wa dansi, baadhi waliuita kwa jina la ‘Mayasa’ na wengine ‘Uzuri ni wa Kuzaliwa Nao’, ilimradi kila mmoja aliweza kufikisha hisia zake kule alikolenga.

Kibao ‘Uzuri ni wa Asili’ au ‘Mayasa’  ulikuwa kama onyo kwa wanawake ambao wanatumia dawa za kujichubua wakitaka kuwa weupe, rangi ambayo ni tofauti na ile ya asili yao ambayo wamezaliwa nayo .

Mwandishi wa makala haya aliwahi kuzungumza na mmoja wa wanamuziki, Hamisi Pishuu, ambaye alikuwa mpiga rhythm wa Dar International alisema wimbo huo ulisababisha mashabiki wa kike kupigana ukumbini.

Nanukuu kauli ya Pishuu:

“Nikiwa na Dar International katika moja ya ziara ya kimuziki mkoani Tabora, wakati tukitumbuiza kwenye ukumbi mmoja, Marijani aliimba wimbo ‘Uzuri wa Asili’. Kibao hicho kiliwagawa wanawake ukumbini hapo katika makundi mawili.

“Kundi la kwanza lilikuwa la wanawake waupe na la pili wanawake weusi. Wanawake  weusi wakawa wanawanyooshea vidole wale wanawake weupe, wakidai  kuwa wamejichubua.

“Wale weupe baada ya kubaini kuwa wanasemwa wao walikuja juu na ndipo hapo zogo kubwa lilipozuka na baadaye walipatanishwa,” mwisho wa kunukuu.

Baadhi ya maneno ya wimbo huo ni haya:

Mayasa mbona wanivunja mbavu mie, sura yako mbona sasa imekuwa hivyoo, ninakuuliza hata kunijibu hutaki, umenikasirikia kama mimi ndiye niliyekutuma, Mayasa hapo zamani haukuwa hivyooo.

Dada yako juzi alikuja kunieleza kwamba umetumia madawa ya urembo, mawazo yako uwe mzuri kuliko ulivyoumbwa, kaniambia umezidisha madawa ya urembo, ukaona bado ukatumia madawa ya nywele, Mayasa sasa ona ulivyo haribikaa. Oh Mayasa  hapo zamani haukuwa hivyoo, oh oh Mayasa, dada Mayasa, uzuri ni wa kuzaliwa nao.

Tuonane wiki ijayo


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*