googleAds

ZAHERA: NAJUA NINI YANGA WANATAKA

NA DAMIAN MASYENENE, MWANZA

HABARI ndiyo hiyo, kama ukichukia chukua kamba ujinyonge maana kauli aliyoitoa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, lazima itawakera wapinzani wa klabu hiyo ya Jangwani.

Baada ya Yanga kupata sare ya bao 1-1 na Pamba katika mchezo wa kirafiki uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa, wapo walioiponda timu hiyo, wakidai kikosi hicho na kocha wake, si lolote.

Wapo wanaokiponda kikosi cha Yanga na wachezaji wake, wakidai baada ya kuvuna fedha za kampeni ya uchangiaji uliofanywa na wapenzi wa klabu hiyo, walitegemea wangesajili wachezaji wa kiwango cha juu, lakini haikuwa hivyo.

Kati ya wachezaji wapya waliotua Yanga kipindi cha usajili kilichopita, ni Lamine Moro pekee aliyeonekana kuwakuna zaidi wapenzi wa soka, akifuatiwa na Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama kipa Mechata Mnata.

Lakini wakati watu wakiwaponda wachezaji wengine wapya wa Yanga, Zahera mara zote amekuwa akiwakingia kifua akidai kinachowaathiri ni mazingira, akiamini baada ya muda si mrefu, wataanza kuonyesha makeke yao.

Na baada ya juzi kuichapa Toto African ya hapa mabao 3-0 CCM Kirumba, Zahera ameibuka na kusema kuwa wale wapinzani wa timu yake waendelee kuwaponda wachezaji na kikosi chake kwa ujumla akitamba binafsi hilo halimuumizi kichwa kwani anafahamu nini Wanayanga wanataka.

Akizungumza na BINGWA juzi baada ya mchezo huo dhidi ya Toto African ambao straika wake, David Molinga alifunga mabao mawili, Zahera alisema: “Hatuchezi mechi za kirafiki kupata matokeo mazuri kumfurahisha kila mtu, bali naangalia ni namna gani mbinu zangu na maelekezo yangu yanafuatwa na wachezaji wangu ili niwape mashabiki wa Yanga kile wanachotarajia kutoka kwangu.”

Alisema ndiyo maana katika mchezo dhidi ya Toto Africans, aliwafanyia mabadiliko wachezaji saba walioanza kipindi cha kwanza kwa sababu walishindwa kutekeleza ipasavyo yale aliyoyaelekeza licha ya kumaliza dakika 45 wakiongoza kwa mabao 2-0.

Mkongomani huyo alibainisha kuwa kwake ushindi siyo lazima kwenye michezo ya namna hiyo (kirafiki), bali namna gani timu inacheza, wachezaji wanajipanga na kutekeleza mipango ya klabu.

“Ushindi siyo lazima, sitafuti ushindi bali namna gani timu inacheza, wachezaji wanajipanga na kutekeleza mpango wangu…. Unaona nilifanya mabadiliko ya wachezaji saba kipindi cha pili kwa sababu hawakucheza kama nilivyoelekeza.

“Najua namna gani nitacheza na Zesco na siyo kama tulivyocheza leo ama juzi (dhidi ya Pamba), najua akina nani wataanza na akina nani hawaanzi….hizi mechi naona washambuliaji wangu wamebadilika sana hata Juma (Balinya) amecheza vizuri sana tofauti na siku za nyuma nadhani ni sababu ya kukaa benchi ama ame improve kisaikolojia,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*