googleAds

Zahera, Lwandamina watambiana

NA WINFRIDA MTOI

MAKOCHA wa Yanga na Zesco, wametambiana kuelekea mchezo wao wa leo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga wanakutana na Zesco baada ya awali kufanikiwa kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, wakitoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam kabla ya kushinda bao 1-0 ugenini.

Ushindi huo ulikuwa ni furaha kubwa kwa Wanayanga, hasa baada ya kusikia watani zao Simba waliokuwa wanatamba kufika fainali, wameondolewa katika michuano hiyo na UD Songo, tena kwenye uwanja wa nyumbani.

Hali hiyo iliwaongezea mzuka Yanga na kuweka mikakati ya kila aina kuhakikisha wanamaliza mchezo wa Zesco nyumbani kabla ya mechi ya marudiano.

Hivyo katika maandalizi waliyofanya Wanajangwani hao, lengo ni kuendeleza furaha hiyo, huku wakicheza mechi za kirafiki kuweka sawa kila idara.

Yanga inaingia uwanjani ikiwa inatambua Kocha Mkuu wa Zesco, George Lwandamina aliwahi kukinoa kikosi hicho, lakini Mwinyi Zahera ameweka wazi mbinu atakayotumia kuing’oa miamba hiyo ya Zambia.

Zesco wanakutana na Yanga baada ya kuitoa Green Mamba ya Eswatini kwa idadi ya mabao 3-0, ilishinda bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Zambia, mchezo wa pili ikashinda 2-0 ugenini.

Historia inawabeba Zesco katika michuano hiyo, kwani mwaka jana Zesco walifika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa upande wa Yanga kwa miaka ya hivi karibuni wanaishia hatua za awali na msimu 2017/2018 waliangukia Kombe la Shirikisho, wakafika hadi makundi.

Makocha wa timu zote mbili wameweka bayana kuwa hawawezi kuangalia historia iliyopita bali wamejipanga kwa  mchezo wa wakati huu.

Akizungumzia mechi hiyo, Zahera wa Yanga, alisema anaifahamu hitoria ya Zesco katika michuanoa hiyo, imeshiriki mara nyingi, lakini yeye ni mwalimu anajua njia gani atapita kupata ushindi.

Zahera alisema hadi kufikia leo ameosoma vya kutosha Zesco, kupitia video za michezo yake ya Ligi Kuu Zambia na ile ya Afrika.

“Nimekuwa nikikaa na wachezaji wangu, tunapitia video za wapinzani, tulifanya hivyo hata kwa Township Rollers, naamini maandalizi yametosha sasa,” alisema Zahera.

Alieleza kuwa tatizo lililokuwa linawasumbua wachezaji wake ni kufunga mabao, ila nafasi wanatengeneza nyingi, kitu alichofanyia kazi na huenda akatumia mfumo mpya.

Kwa upande wake Lwandamina alisema alikuwepo Yanga, lakini hiyo haimfanyi ajiamini kushinda kwa sababu kikosi kimebadilika na benchi la ufundi ni jipya.

“Tunaingia katika mchezo kutafuta ushindi, si kwa sababu niliwahi kuwa mwalimu wa Yanga, bali kutumia mbinu zangu za sasa na wachezaji nilionao kusaka ushindi,” alisema Lwandamina.

Yanga jana ilifanya mazoezi yake ya mwisho katika viwanja vya Gymkhana, Dare es Salaam.

Kikosi cha Yanga kinachotarajia kuonekana leo ni kipa Farouk Shikalo, Fei Toto, Tshishimbi, Lamine Moro na Kelvin Yondani.

Wengine ni Ally Mtoni ‘Sonso’, Mapinduzi Balama, Juma Balinya, Sadney Urikhob na Juma Balinya, Abdulaziz Makame na Patrick Sibomana.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*