ZAHERA KUTUMIA MIKANDA YA VIDEO KUIUA MTIBWA

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amesema anatarajia kukaa na wachezaji wake leo kuangalia video za mchezo wao wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ili waone makosa waliyofanya kabla ya kuvaana na Mtibwa Sugar.

Juzi Yanga walicharuka na kutamba nyumbani baada ya kuwafunga waarabu hao kutoka nchini Algeria mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga wanatarajia kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumenyana na Mtibwa Sugar keshokutwa katika dimba la Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Zahera alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuwapa maelekezo wachezaji wake kwa vitendo ili wajue makosa yao na yasijirudie kwenye mechi ya Ligi Kuu watakapokutana na Mtibwa.

Aidha, kocha huyo aliwapongeza wachezaji wake kwa kile walichokifanya huku akieleza kuwa kama mwalimu amebaini kuna makosa mengi waliyofanya ambayo hatapenda yaendelee kuonekana katika mechi zijazo za ligi.

“Kila mchezaji hakucheza kwa asilimia 100, kuna  makosa wamefanya licha ya kwamba tumefanikiwa kushinda, hivyo nitachukua mkanda wa video ya  mchezo wetu dhidi ya USM Alger ili niwaelekeze kwa vitendo,” alisema Zahera.

Hata hivyo, aliongeza kwamba jambo linalompa moyo zaidi na kuamini atafanikiwa kukiweka sawa kikosi hicho ni ushirikiano unaendelea kuonyeshwa na wachezaji uwanjani.

“Napata moyo wa kuendelea kukiimarisha kikosi kwa sababu ya umoja wa wachezaji uwanjani, kipindi wakiwa na mpira na hata wakati hawana mpira wanafanya kazi kwa ushikiano,” alieleza Zahera.

Zahera alifafanua kuwa suala la kuangalia makosa kwa kutumia video za mechi litakuwa endelevu kwani litasaidia kufuta makosa kwa haraka endapo mchezaji hajamuelewa mazoezini.

Pia aliwataka Wanayanga kuendelea kuivumilia timu yao kwani inafanya kazi kubwa na baada ya wiki tatu watakuwa katika kiwango bora zaidi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*