Zahera hana mpinzani Yanga

NA HUSSEIN OMAR                  

KWA yeyote akisema Mwinyi Zahera hana mpinzani ndani ya Yanga, hatakuwa amekosea baada ya Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Samwel Lukumay, kumtaka kocha huyo kutosikiliza maneno ya watu na badala yake apige kazi.

Kauli ya Lukumay imekuja siku chache baada ya Zahera kuanza kupigwa mizengwe na watu wachache wanaodaiwa kutoitakia mema klabu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Zengwe hilo linatokana na msimamo mkali uliowekwa na kocha huyo ambaye alisisitiza fedha zote zinazotokana na michango ya wanachama, wadau na mashabiki wao, ziingizwe kwenye akaunti maalumu ili kuisaidia timu hiyo inayokabiliwa na ukata kwa sasa.

Msimamo wa kocha huyo raia wa DR Congo, unaonekana kuwakera baadhi ya vigogo ambao hawamkubali hivyo kuanza kumpiga mizengwe kutaka aondoke.

Akizungumza na BINGWA Dar es Salaam jana, Lukumay alisema wao kama viongozi wamekaa na kocha huyo na kumtaka kutosikiliza maneno ya watu badala yake apige kazi.

“Tumeongea na mwalimu tumemwambia haya mambo yapo, lakini anatakiwa asiyaweke sana moyoni kwake, afanye kazi yake kwa bidii kuipa mafanikio Yanga,” alisema Lukumay.

Alisema wamempa baraka zote kocha huyo kufanya mambo mema yenye masilahi na tija ndani ya Yanga na kumtaka kutokata tamaa na maneno maneno ya watu yanayosemwa mtaani.

Kocha Zahera kwa sasa ndiye kila kitu ndani ya Yanga, kwani uwepo wake umeifanya timu hiyo ikusanye pointi 54 baada ya kushinda michezo 18 kati ya 21 iliyocheza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*