ZAHERA AWAWEKA NDANDA KIGANJANI

NA SAADA SALIM


KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, hana presha na wapinzani wake wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ndanda FC, baada ya kuwafuatilia katika michezo yao kadhaa.

Yanga wanatarajia kucheza na Ndanda FC kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Zahera kuweka wazi kwamba hawatatoka salama kutokana na  programu aliyowapa nyota wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana katika Makao Makuu ya Klabu ya Yanga, Zahera alisema amepata nafasi ya kuwasoma wapinzani wake katika mechi mbili ikiwamo dhidi ya Simba na ile ya KMC na kujua anachotakiwa kufanya katika kikosi chake.

Zahera alisema anafahamu kuwa timu hizo ndogo zinapocheza na kubwa huwa zinajituma na kukamia, hivyo amejua jinsi ya kuwadhibiti ili kupata pointi tatu muhimu.

“Nimewapa programu ngumu wachezaji wangu kwa kuhakikisha wanajituma, kuhusu tunahitaji mabao mangapi kikubwa ni kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,” alisema.

Alisema kuelekea mchezo huo atawakosa wachezaji wake watatu, Kelvin Yondani aliyeumia katika mchezo uliopita, Papy Tshishimbi na Paul Godfrey aliyepewa kadi nyekundi katika mchezo dhidi ya Lipuli FC.

“Nitawakosa wachezaji hao, lakini Ibrahim Ajib na Andrew Vicent ‘Dante`, tayari wameshaanza mazoezi, hivyo kuna uwezekano wakawepo katika kikosi, nafasi ya Paul sina presha baada ya Juma Abdul kurejea katika nafasi yake.

“Baada ya Paul kumaliza adhabu, atarejea katika kikosi cha kwanza hata kama Juma Abdul atakuwa vizuri, kwani sihitaji kushusha morali ya kijana huyo ambaye amefanya vizuri sana tangu mechi ya Simba nilipompa majukumu,” alisema.

Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, ametangaza viingilio vya mchezo huo kwa kiwango cha juu ni Sh 15,000, Sh10, 000 na Sh 5000.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*