ZAHERA ANAPOTUKUMBUSHA DAWA YA MOTO NI MOTO

NA AYOUB HINJO


WAPO wanaoamini na kuishi kwa kutukuza misemo, ndio hao wapo karibu mahali kote duniani, tena hufuatilia kwa ukaribu kweli kweli ili kupata njia mpya za kuishi.

Pia, moja ya misemo ambayo imekuwa ikitumika hapa nchini ni dawa ya moto ni moto, maana yake ubaya unalipizwa kwa ubaya na kinyume chake.

Napenda kumsikiliza Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, anavyozungumza kuhusu mchezo au hata wachezaji wake walivyocheza katika mechi husika, wala haihitaji kupindisha ukweli, atasema kila kitu kwa uwazi kabisa.

Huyo ndiye Zahera, ambaye kwa hapa nchini taratibu ameanza kuchokwa na mashabiki wa Yanga ambao wanaamini kocha huyo anaongea mambo ambayo yalipaswa kuwa siri baina yake na wachezaji.

Pamoja na hayo yote, Yanga imekuwa ikipata matokeo ya ushindi katika kila michezo nane waliyocheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wakishinda saba na kutoa sare mmoja dhidi ya Simba.

Yanga ambayo haikupewa nafasi ya kufanya vizuri msimu huu kutokana na ukata ulioizunguka timu hiyo, walisajili kwa kuungaunga tena, ikikumbukwa hata baadhi ya wachezaji walipewa kutoka Singida United.

Kwa jinsi taswira yao ilivyokuwa ilikuwa ngumu kuwawekea dhamana ya ushindi, lakini kadiri muda unavyozidi kusogea mbele wamekuwa wakibadilika taratibu.

Wanakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, nyuma ya Azam kwa michezo miwili, kwa maana hiyo kama wakicheza mechi hizo mbili na kushinda wataongoza ligi kando ya Simba na Azam, waliotajwa kuwa bora zaidi msimu huu.

Lakini hayo yote yanatokea sababu ya uwepo wa Zahera ndani yake, kwa mara ya kwanza nilipokutana naye alipotembelea ofisi za gazeti hili, Sinza Kijiweni, alionekana kuwa mtu makini na mwenye kufuatilia kila hatua.

Zahera hapendi wachezaji wavivu, lakini anavutiwa zaidi kama mchezaji atacheza kwa kufuata kile anachokihitaji kwa muda wote katika mchezo husika.

Hana tofauti na Jose Mourinho, sababu haoni kazi kumzungumzia mchezaji wake kwa uwazi zaidi mbele ya waandishi wa habari bila kujali itamwathiri au itamsaidia.

Ibrahim Ajib ni mhanga mkubwa wa Zahera, katika kipindi ambacho inaaminika mchezaji huyo wa zamani wa Simba yupo katika ubora mkubwa, lakini kwa kocha huyo bado hajaonyesha kitu chochote, licha ya kuisaidia timu.

Katika michezo nane ya Yanga, Ajib amefunga mabao matatu na kutoa asisti zaidi ya sita, achana na msemo wa namba hazidanganyi, hicho kitu kwa Zahera hakipo kabisa.

Licha ya umahiri mkubwa aliokuwa nao Ajib uwanjani, bado si kitu kwa kocha wake ambaye mara kadhaa amezungumza juu ya uwezo wa mchezaji huyo mbele ya waandishi wa habari.

Katika kipindi ambacho wadau wa soka hapa nchini waliamini ni muda sahihi wa Ajib kujumuishwa kwenye kikosi cha timu Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwa Zahera imekuwa kinyume. Si Ajib pekee, hata akina Papy Tshishimbi na Heritier Makambo wote wameingia katika anga za kocha huyo na kuwaanika kwa waandishi wa habari bila woga wowote.

Hivi karibuni tu, alisema Makambo anacheza vibaya sababu hapati muda mwingi wa kupumzika, mwili wake unakosa muda wa kutulia kwa kusisitiza kabisa alikazia kuwa taratibu anaweza kujikuta benchi na ikiwezekana ataishia kukaa jukwaani.

Huyo ndiye Zahera, ukimfurahisha atakuambia na ukimkera hatasita kusema hilo.

Kwa kila anachokifanya kocha huyo raia wa DR Congo, kinaonekana kigeni hapa kwetu na kuwafanya mashabiki kumwona anafanya makosa makubwa kuongea hivyo.

Binafsi naona kuna mambo Zahera anayahitaji kutoka kwa wachezaji wake.

Kuongea kwa uwazi juu ya Ajib, Tshishimbi na Makambo au wengine ni ishara kuwa kocha huyo anahitaji wachezaji wake kucheza kwa kiwango cha juu kila Yanga inapokuwa uwanjani.

Katika mchezo ambao Ajib anatoa pasi tatu au mbili za mabao na kufunga, anatuambia amecheza ovyo, maana yake kuwa kwenye mchezo ujao afanye juhudi zaidi.

Wasiwasi wangu upo kwa wachezaji wake kama wanamwelewa anachokihitaji kocha huyo, inawezekana likapita kwenye sikio moja na kutokea kwingine.

Kwa wenzetu huko Ulaya, hilo ni jambo la kawaida sana kwao, mara ngapi Mourinho au makocha wengine huongea kwa uwazi juu ya maendeleo au kuporomoka kwa wachezaji wao? Ni mara nyingi sana.

Zahera haongei kumfurahisha mtu au waandishi wapate habari, anaongea kuwafanya wachezaji wawe na upeo na kutambua kazi yao kila wanapokuwa uwanjani au nje.

Inawezekana kuna viongozi wanachukizwa na maneno ya Zahera, lakini wakiangalia mwendo wa timu yao umekuwa wa kuridhisha zaidi, watafanya nini zaidi ya kuchukia kumpenda kocha huyo.

Kadiri muda unavyokwenda nafsi zao zinazidi kuchukia kumpenda kocha huyo, lakini kama timu inapata matokeo kila inapoingia uwanjani hakuna tatizo kwao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*