googleAds

ZAHERA AMPIGA BAO MBELGIJI WA SIMBA

NA WINFRIDA MTOI

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ametwaa tuzo ya kocha bora wa Septemba, huku Amri Said wa Mbao FC akichukua ya mwezi Agosti.

Zahera ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Zuberi Katwila wa Mtibwa Sugar na Bakari Shime wa JKT Tanzania, alioingia nao fainali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema Kamati ya Tuzo ya Ligi Kuu Tanzania Bara imemchagua Zahera kutokana na kushinda michezo mitatu katika mwezi huo.

Kwa upande wa Said wa Mbao, aliwashinda Patrick Aussems wa Simba na Hans van Pluijm wa Azam FC, alioingia nao fainali. Kocha huyo aliiwezesha Mbao kushinda michezo miwili na kutoka sare moja, wakati Pluijm aliiwezesha timu yake kushinda michezo miwili, sawa na Aussems wa Simba.

 

Alisema Katwila aliingia fainali baada ya kuiwezesha Mtibwa kushinda michezo mitatu, huku Shime akishinda mechi mbili.

Ndimbo alisema tuzo hiyo ni mpya na itakuwa ikitolewa kila mwezi kwa kocha atakayefanya vizuri. Wakati huo huo, mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile, ameibuka mchezaji bora wa Septemba, baada ya kuwashinda Ibrahim Ajib wa Yanga na Stamili Mbonde wa Mtibwa Sugar.

Ndimbo alisema Ambokile ametwaa tuzo hiyo kwa kuonyesha kiwango kikubwa kwa mwezi huo na kufunga mabao manne katika mechi tano Mbeya City ilizocheza.

Alisema kutokana na ushindi huo, Ambokile atazawadiwa Sh milioni moja na kisimbusi cha Azam TV, huku makocha wakipewa tuzo pekee.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*