YANGA YAPETA ETHIOPIA, NSAJIGWA KUFANYA ‘SURPRISE’ YA KIKOSI

NA HUSSEIN OMAR   |   

WACHEZAJI wa Yanga wakiongozwa na Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Papy Kabamba ‘Tshishimbi’, jana asubuhi wamepiga tizi la kufa mtu katika Uwanja wa Awassa, kujiandaa na mchezo wao wa marudiano dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia kesho, wakipania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Yanga kiliondoka nchini juzi alfajiri kwenda Ethiopia na kutua salama katika mji wa Awassa na kesho watashuka dimbani kumalizana na Dicha ambao katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa     Taifa, Wanajangwani hao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Ili kutinga hatua ya makundi, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi kitu ambacho kimewafanya nyota wa timu hiyo na benchi la ufundi likiongozwa na Noel Mwandila, kutokuwa na wasiwasi na mchezo huo wa kesho.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kikosi cha timu hiyo kipo vizuri na jana asubuhi walitumia muda wa saa moja kufanya mazoezi ya kutembea katika mitaa mbalimbali ya mji huo kwa ajili ya kuweka miili yao sawa kabla ya jioni kufanya mazoezi ya uwanjani.

“Tupo vizuri na hakuna shaka yoyote, tumepokewa vizuri hakuna figisu figisu zozote zilizotokea, kwa kweli tumepata faraja kubwa sana kuona kuna Watanzania wenzetu huku wanatupa sapoti, imebaki kazi moja tu ya uwanjani kupata matokeo,” alisema Hafidh.

Alisema katika kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wa timu hiyo, Mwandila ambaye amekabidhiwa mikoba ya George Lwandamina, tangu wamefika nchini humo amekuwa akitumia muda mwingi kuzungumza na wachezaji wake kuhusiana na mchezo huo wa kesho na kuwaandaa kisaikolojia.

“Kimsingi wachezaji wamekuwa wakiandaliwa zaidi kisaikolojia, ukizingatia tumefikia katika hoteli nzuri ya Rori Holiday, ambayo mazingira yake ni rafiki kukaa mchezaji,” aliongeza Hafidh.

Katika hatua nyingine, wachezaji wa timu hiyo jana walipiga tizi la kufa mtu wakichagizwa na meseji ya kuwatakia kila la  kheri iliyotumwa na Kocha wao Lwandamina na kuahidi kushinda mchezo huo ili waweze kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Nahodha wa Yanga, Cannavaro, aliliambia     BINGWA     kuwa     hakuna namna nyingine ya kutinga hatua ya makundi zaidi ya kushinda mchezo huo na kuwataka wachezaji wenzake kuweka historia nyingine kwa Wanajangwani hao.

“Tunahitaji ushindi hatukuja hapa kutafuta sare, tumekuja kuandika historia nyingine Afrika kwa kutinga hatua ya makundi kwa kishindo,” alisema Cannavaro.

Kwa upande wake, Yondani alisema wana kila sababu ya kufanya kweli kwenye mchezo huo wa kesho na kuwataka mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kujiandaa kuwapokea kwa kishindo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, pindi watakaporejea nchini.

“Wajiandae kuja kutupokea kwa kishindo, uwezo wa kutinga hatua ya makundi tunao,” alisema Yondani.

Kikosi kamili huenda kikapangwa kama ifuatavyo:-

Youthe Rostand, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Yondani, Cannavaro , Kamusoko, Yusuph Mhilu, Tshishimbi, Pius Buswita, Obrey Chirwa na Emanuel Martin.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*