googleAds

Yanga yapata katibu mkuu mpya msomi

ASHA KIGUNDULA NA ZAINAB IDDY

KAMATI ya Utendaji ya Yanga chini ya mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla, imempitisha msomi wa ugavi Dk. David Ruhago kuwa katibu mpya wa klabu hiyo.

Ruhago alipitishwa katika kikao cha kamati hiyo, iliyokutana jijini Dar es Salaam juzi usiku, kujadili masuala mbalimbali, ikiwamo mchezo wa Ligi Mabingwa Afrika dhidi ya ZESCO ya Zambia, utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, kilimpitisha Hassan Bumbuli kuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, akichukua nafasi ya Dismas Ten aliyemaliza mkataba wake.

“Katika nafasi ya katibu mkuu wajumbe wengi waliridhishwa na wasifu wa Ruhago, ambaye ni mwanayanga mwezetu  kwa kipindi kirefu kutokana na kufanya kazi mbalimbali kwenye kamati mbalimbali  za Yanga, akiwa na kiwango kizuri cha elimu.

 “Tunataka Yanga iendeshwe na watu wenye elimu na mipango ya maendeleo na kwa kuwa katibu mkuu ndio mtendaji wa kila kitu Ruhago amestahili  kwa sifa hizo,”alisema mtoa habari yetu.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alikiri kamati ya utendaji  kuketi na kupitisha maamuzi mbalimbali.

 “Ni kweli jana (juzi) kamati ya utendaji ilikutana kujadili mchezo wetu na ZESCO,  lakini pia kufanya uteuzi wa katibu mkuu na msemaji.

“Taarifa rasmi juu ya nani ataajiriwa katika nafasi ya katibu mkuu na mkuu wa kitengo cha habari zitatolewa hivi karibuni kwa sababu kuna kamati mpya ya uhamasishaji imeundwa nayo inatakiwa kutangazwa,”alisema Mwakalebela.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*