googleAds

YANGA YANOGESHA UBINGWA

NA WAANDISHI WETU,

YANGA hawataki utani, kwani baada ya kuona kila dalili za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wameamua ‘kuwaroga’ zaidi wachezaji wao kwa kuhakikisha wanawalipa madeni yao yote ya mishahara kama sehemu ya kunogesha sherehe za ubingwa unaonukia Jangwani.

Bila shaka hizo zitakuwa ni habari njema kwa wachezaji wa timu hiyo ambao walijikuta wakiwa katika wakati mgumu kutokana na kutolipwa mishahara ya miezi mitatu.

Akizungumza na BINGWA jana, mmoja wa vigogo wa timu hiyo anayeunda Kamati ya Utendaji, alisema tayari mipango ya kuwalipa nyota wao imekamilika.

“Mwenyekiti ameomba kupewa majina ya wachezaji wote wanaodai mishahara yahakikiwe ili aweze kumalizana nao mara moja,” alisema kiongozi huyo.

Alisema katika kipindi cha miezi miwili mpaka mitatu iliyopita, klabu yao ilikuwa katika mtikiso mkubwa wa kiuchumi na kusababisha kuwapa wakati mgumu wachezaji wao ambao hata hivyo, waliweka matatizo yao pembeni na kuipigania timu katika mbio za kusaka ubingwa.

Akithibitisha hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface, alikiri kila mchezaji anayedai mshahara kulipwa fedha zake ndani ya siku chache zijazo.

“Hapa katikati tuliyumba kidogo kiuchumi, lakini kwa sasa utaratibu unaandaliwa kwa ajili ya kuwalipa mishahara wachezaji wote, mpaka ligi ikishamilizika, tuwe tumeshamalizana nao,” alisema Mkwasa.

Hilo linatokea ikiwa ni siku chache tangu kampuni ya mashindano ya bahati nasibu ya SportPesa kuingia mazungumzo na Yanga kwa lengo la kuwadhamini ambapo imedaiwa kuwa, timu hiyo imetoa masharti ili iweze kuwa tayari ‘kufunga ndoa’ na kampuni hiyo.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa, ili waingie mkataba na kampuni hiyo, wameitaka SportPesa kutoa kiasi cha Sh milioni 140 kwa mwezi, basi la kusafiria, jezi zenye ubora wa hali ya juu pamoja na kuwatengenezea uwanja wa mazoezi.

“Baada ya SportPesa kuweka dau lao mezani, uongozi wa juu ulikaa kujadili kisha kupeleka kile walichokipendekeza kwa bosi mkubwa ili kuidhinisha, ndipo yalipokuja mapendekezo hayo.

“Iwapo SportPesa watakubali hilo, basi tupo tayari kuingia mkataba na kampuni hiyo,” alisema mtoa habari huyo.

Juu ya masharti hayo ya Yanga, Bingwa lilimtafuta Abbas Tarimba kuzungumzia hilo ambapo alisema: “Mimi sifahamu hilo, kama kuna mapendekezo hayo bado hayajanifikiwa, hivyo siwezi kuzungumza lolote.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*