Yanga yamtafuta ubaya Mo


*Kwa walichopanga kukifanya, Wekundu wa Msimbazi lazima walie Ligi Kuu Bara

NA ZAITUNI KIBWANA

ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya Yanga kuvaana na Biashara United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Mwinyi Zahera, ametamba kuendeleza ushindi lengo likiwa ni kuzidi kujikita kileleni mwa kipute hicho hadi mwisho.

Kauli hiyo ya Zahera huenda zikawa ni habari mbaya kwa watu wa Simba, akiwamo mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘MO’, ambao wanatamani kukiona kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao kikiendelea kutamba kwa kutetea ubingwa wao.

Japo Mo na mabosi wenzake wa Simba akili yao ni kuipa timu yao mafanikio katika anga ya kimataifa, lakini hawawezi kuudharau ubingwa wa Bara unaowapa tiketi ya kushiriki michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Ikumbukwe kuwa Simba ilihaha misimu mitano kuusaka ubingwa wa Bara bila mafanikio kabla ya kubeba ‘mwali’ msimu uliopita, ikiwa ni baada ya Yanga kutamba ndani ya kipindi hicho, ikibeba kombe mara nne na Azam mara moja.

Akifahamu pengo la pointi lililopo baina yao na Simba, yaani pointi 11, Zahera aliliambia BINGWA kuwa amejizatiti kuhakikisha hawashuki kileleni mwa ligi hiyo kwa kushinda mechi zao zote zijazo, ikiwamo dhidi ya Biashara United wikiendi hii ili mwisho wa siku waweze kuurejesha ubingwa wa Bara Jangwani.

Akizungumzia mchezo wao huo unaofuata utakaopigwa Jumapili, Zahera alisema: “Kikosi chetu kipo fiti na tayari kwa mechi zote za ligi kuu zinazofuata, ikiwemo ya wikiendi hii dhidi ya Biashara United. Tumejipanga kuibuka na pointi tatu ili tuendelee kujiweka pazuri.”

Alisema baada ya kikosi cha Yanga kurejea Dar es Salaam jana mchana kikitokea mkoani Mbeya kilipocheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, kikosi chake kinatarajia kuingia kambini leo kuanza maandalizi ya kuivaa Biashara United.

Katika hatua nyingine, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, amesema kambi hiyo wataitumia vema kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo na mingine minne inayofuata kuhakikisha wanashinda yote ili watwae ubingwa wa ligi hiyo.

Baada ya kushuka dimbani mara 14, Yanga wamejikusanyia pointi 38 huku Simba waliocheza mechi 12, wakiwa na 27, wakishika nafasi ya tatu nyuma ya Azam waliojikusanyia pointi 35 kutokana na michezo 14.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*