googleAds

Yanga yampa mtihani Zahera

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa Yanga umesema hawatakuwa na sababu yoyote kwa timu yao kufungwa katika michuano ya kimataifa, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutuma leseni ya kipa wao,  Farouk Shikalo.

Shikalo aliyesajiliwa na Yanga dakika ya mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la Caf Julai 31, mwaka huu, hakutumika katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kutokamilika kwa usajili wake.

Kipa huyo, anatarajiwa kuwapo katika kikosi cha kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera kitakachocheza na ZESCO ya Zambia keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijiji Dar es Salaam.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema kwa sasa Zahera hatakuwa na sababu ya  timu  hiyo kufungwa baada ya Shikalo leseni ya kuitumikia klabu yao.

Mwakalebela alisema Shikalo ambaye wamemsajili kutoka  Klabu ya Bandari ya Kenya ni kipa mzuri mwenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.

Alisema leseni ya kipa wao  ilitumwa juzi, hivyo Zahera atakuwa na uamuzi wa kumtumia mchezo wa keshokutwa dhidi Zesco.

“Suala la kumtegemea kipa mmoja lilituumiza kichwa  na tulipaswa kumuomba Mungu ili asipate  tatizo, lakini  Metacha (Mnata) alitimiza majukumu yake kikamilifu kwenye mechi za kimataifa.

“Kabwili yupo,  lakini tulimtegemea zaidi kwenye mechi za  Ligi Kuu na si kimataifa, juzi tumepokea taarifa za kuruhusiwa kucheza kwa Shikalo kwenye mechi yetu inayokuja, hii ni habari njema kwetu,”alisema Mwakalebela.

Alisema: “Tulipambana kuhakikisha leseni yake inakuja na tumefanikiwa, kazi iliyopo ni kocha Zahera kuamua nani wa kumpanga ili tusiweze kuruhusu kufungwa .


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*