Yanga yafunga barabara Moro

*Watua mjini humo kibabe, waanza mazoezi fasta fasta

*Sibomana, Marcelo, Kalengo, Balinya kama wafalme

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

KIKOSI cha Yanga kimetua mjini Morogoro jana kwa mbwembwe, huku mashabiki wake wakijazana kandokando ya barabara kuwalaki wachezaji wao, waliowasili hapa kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao.

Katika maeneo yote ambayo basi la Yanga lilipita, mashabiki wao walikuwa wakiwashangilia vilivyo, huku wakionekana kuwa na shauku ya kuwaona wachezaji wao wapya, hasa wale wa kigeni.

Kati ya wachezaji waliokuwa wakitajwa zaidi na mashabiki, ni Patrick Sibomana (Rwanda), Issa Bigirimana (Burundi), Maybin Kalengo (Zambia), Juma Balinya (Uganda) na Farouk Shikalo (Kenya) ambaye hata hivyo bado hajaungana na kikosi cha Yanga, akiitumikia klabu yake ya Bandari katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’, nchini Rwanda.

Kwa upande wa wazawa, waliokuwa wakitajwa zaidi ni Abdulaziz Makame, (Mafunzo), Muharami Issa Said (Malindi FC), Metacha Mnata (Mbao FC) na Balama Mapinduzi (Alliance)

Mara baada ya kutua katika hoteli watakayoweka kambi ya Kings Way iliyopo Msamvu, wachezaji walipumzika kabla ya kupata chakula cha mchana na kisha kuelekea mazoezini katika Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini hapa.

Mazoezi hayo yalifanyika chini ya kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, wakati huu ambao bosi wake, Mwinyi Zahera, akiwa mapumzikoni nchini Ufaransa, baada ya kikosi cha DR Congo kutolewa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) kwa kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-2 na Madagascar juzi.

Akizungumza na BINGWA jana, Mratibu wa kikosi cha Yanga, Hafidh Saleh, alisema: “Tumeshafika Morogoro na leo (jana) jioni tutaanza mazoezi, lakini kesho (leo) kocha atapanga vizuri programu kama watafanya mara mbili kwa siku au moja.”

Alisema baada ya timu ya DR Congo kutolewa katika michuano ya Afcon2019, wanatarajia Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu yake hiyo ya taifa, atawasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kuendelea na programu ya mazoezi.

Saleh alisema wamewapa mapumziko ya wiki moja baadhi ya wachezaji wao waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na baada ya hapo, wataungana na wenzao katika kambi hiyo.

Juu ya walivyojiandaa kuitunza timu yao kwa wakati wote itakapokuwapo mjini hapa, Katibu wa Matawi ya Yanga Morogoro, Edward Mhagama, alisema kuwa wameandaa ulinzi ‘bab kubwa’ kuhakikisha kambi hiyo inakuwa tulivu na ya mafanikio kwa wachezaji wao.

“Kama ilivyo kawaida yetu, tumejipanga kila idara kuhakikisha kambi ya timu yetu inakuwa ya mafanikio makubwa, ulinzi umeimarishwa kila timu itakapokuwa, hivyo wapenzi wa Yanga wa Dar es Salaam na kwingineko wasiwe na wasi wasi, vijana wao wapo kwenye mikono salama,” alisema Mhagama ambaye ni miongoni mwa Wanajangwani maarufu hapa nchini.

Wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa na Yanga ni Lamine Moro (Ghana), Mustapha Selemani (Burundi), Sadney Ukhob (Namibia), Bigirimana (Burundi), Sibomana (Rwanda), Shikalo (Kenya), Balinya (Uganda) na Kalengo (Zambia).

Wazawa ni Ally Ally (KMC), Makame (Mafunzo), Marcelo (Malindi), Mnata (Mbao FC) na Mapinduzi (Alliance).

Kwa miaka ya hivi karibuni, Yanga imekuwa na utamaduni wa kuweka kambi Morogoro, ikifanya hivyo pia msimu uliopita.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*