googleAds

Yanga yafanya kufuru Tanga

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

TIMU ya Yanga imetua jijini hapa na kufanya kufuru ya aina yake, kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union unaotarajiwa kuchezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo, Yanga imejichimbia katika hoteli ya bei mbaya jijini hapa ambayo ndiyo inayotumiwa na wageni maarufu, kuanzia viongozi wa serikali, wasanii na wengineo.

Hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano, ni Tanga Beach Resort iliyopo ufukweni wa Bahari ya Hindi.

Sambamba na hilo, mashabiki wa timu ya African Sports ya hapa, wenye ‘undugu’ wa kiasili na Yanga, wameamua kuungana na Wanajangwani hao ili kuwapa njia za kuwawezesha kuifunga Coastal Union.

Ikumbukwe Yanga na African Sports zina uhusiano wa kiasili, huku Coastal Union maswahiba wao wakiwa ni Simba.

Mara baada ya kikosi cha Yanga kutua hapa, ilikutana na mapokezi ya aina yake kutokana na umati mkubwa wa mashabiki na wanachama wao waliojitokeza kuwalaki vijana wao.

Tayari shamrashamra za kuelekea mchezo huo zimeanza huku wauzaji wa jezi wakiwa tayari wamekwisha kuanza kufanya yao katika mitaa mbalimbali ya jiji hili.

Na jana jioni, kikosi cha Yanga kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Popatlaly, chini ya kocha wao, Luc Eymael.

Mazoezi hayo yalifanyika chini ya ulinzi mkali, yakihudhuriwa na mashabiki lukuki, huku baadhi wakizuiwa kuingia uwanjani hapo, ikiwa ni moja ya sehemu ya joto la mchezo huo wa Jumapili.

Akiuzungumzia mchezo huo, Eymael alisema: “Tunacheza na timu nzuri, Coastal Union imepoteza mechi yao iliyopita na walikuwa na matokeo mazuri, hivyo wamejipanga. Lakini nasi tumejipanga kuchukua pointi tatu. Mechi iliyopita tulipata sare, hivyo tuna kila sababu ya kushinda mechi hii.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*