YANGA WAWEKA MKAKATI MZITO

NA HUSSEIN OMAR

HII huenda ikawa isiwe habari njema kwa mashabiki wa Azam kutokana na ukomavu waliouonyesha wachezaji wa Yanga, ambao wameamua kwa kauli moja kukutana jana na kuweka mikakati kabambe itakayowawezesha kuwasambaratisha Wanalambalamba hao katika mchezo baina yao utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa raundi ya 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kufunga mzunguko wa kwanza msimu huu.

Yanga wanafahamu kuwa ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini, ndio utakaowawezesha kurejea kwenye mstari wa kutetea ubingwa wao wa Bara, lakini pia kuwatambia wapinzani wao hao ambao wamekuwa wakiwasumbua mno wanapokutana.

Lakini pia kuna jambo linaloumiza vichwa vya wapenzi na wachezaji wa Yanga kwamba, iwapo Simba itatwaa ubingwa mshambuliaji wao aliyetua Jangwani msimu huu akitokea Msimbazi, Ibrahim Ajib, ataumia mno kwa kejeli atakazokuwa akitolewa na mashabiki wa timu yake hiyo ya zamani.

Kwa kufahamu hilo, mbali ya mikakati ya klabu kwa ujumla, wachezaji wa Yanga jana walikutana na kufanya kikao kizito baada ya mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru, ambapo walikubaliana ‘kufia’ uwanjani Jumamosi dhidi ya Azam, lengo likiwa ni kutoka Chamazi na ushindi.

Iwapo Yanga watashinda mchezo huo, watafikisha pointi 28 na hivyo kuwakaba koo Azam na Simba zilizopo kileleni, Wekundu wa Msimbazi wakiwa na pointi 32 na Wanalambalamba 30 kabla ya mechi zao za wikiendi hii.

Akizungumza na BINGWA jana, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema kuwa wanaupa uzito mkubwa mchezo huo wa Jumamosi ndio maana waliufanyia kikao kizito kupeana mikakati mbalimbali ya ushindi.

“Ni mechi ngumu ambayo tunahitaji kushinda, kwa kutambua hilo, tumeamua sisi kama wachezaji peke yetu kukutana wenyewe bila kumhusisha kiongozi yeyote kuangalia tulikosea wapi michezo iliyopita na nini tunatakiwa kufanya katika mchezo wetu na Azam,” alisema Cannavaro.

Cannavaro alisema ushindi watakaoupata katika mchezo huo, unaweza kuwapa mwanga mzuri kwani watakuwa wamefikisha alama 28 ambazo zinaweza kuwaweka katika nafasi nzuri ya kutetea taji lao.

Katika kutambua umuhimu wa mchezo huo wa Jumamosi, uongozi wa Yanga kupitia Katibu Mkuu wake, Charles Boiniface Mkwasa, umeamua kuwaficha wachezaji wao katika hoteli ya kifahari ya Zimbo iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwasambaratisha Azam.

Katika hatua nyingine, mabingwa hao wa Tanzania Bara jana walifanya mazoezi ya kufa mtu katika Uwanja wa Uhuru, lengo likiwa ni kuwaandaa nyota wake kuelekea katika pambano lao hilo la Jumamosi.

Benchi la ufundi la Yanga likiongozwa  na Kocha Mkuu, George Lwandamina na wasaidizi wake, Shadrack Nsajigwa, Juma Pondamali na Noel Mwandila, walionekana kutilia mkazo zaidi zoezi la umaliziaji na kuwapa mbinu mbalimbali za ufungaji nyota wa timu hiyo.

Lwandamina aliwaelekeza wachezaji wake jinsi ya kufunga kwa kutumia mbinu za kubaki na beki mmoja, mabeki wawili na mabeki wanne na namna ya kukaba pindi wanapopoteza ‘move’ za mabao.

BINGWA lilishuhudia Lwandamina akigawa makundi tofauti tofauti na kuanza kuwapa mbinu za kufunga kumpita beki mmoja kisha baadaye kuwapita wawili kwa kasi kwa ajili ya kutafuta pumzi na mabao.

Katika mazoezi hayo wachezaji wote wa Yanga wakiongozwa na mshambuliaji wao, Obrey Chirwa, walionekana kuwa na morali ya hali ya juu kwenye mazoezi hayo na kufurahia mbinu walizokuwa wakipewa na makocha wao.

Yanga ina kibarua kigumu katika mechi hiyo kutokana na kutofanya vizuri katika mechi mbili zilizopita, ambapo awali ilitoka suluhu 0-0 dhidi ya Mwadui kisha kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa Jumapili iliyopita,   Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*