Yanga waipigia kambi Azam

NA HUSSEIN OMAR

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamepotezea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro juzi Jumatano na kuamua kuingia kambini kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam FC.

YANGA inatarajiwa kuingia kambini kesho kujiandaa na mchezo huo wa Ligi Kuu utakaopigwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga wameutolea macho mchezo huo baada ya kupoteza dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro na sasa wanajipanga kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

Kocha wa kikosi hicho cha Yanga, Mwinyi Zahera, alisema tayari amewaambia vijana wake wasikate tamaa, licha kupoteza dhidi ya Mtibwa.

“Mchezo dhidi ya Azam FC ni muhimu sana, ingawa tunaiheshimu timu hiyo, ila tunajipanga kupambana kuhakikisha tunabeba pointi tatu ambazo ni muhimu katika mbio za ubingwa,’’ alisema Zahera.

Alisema kesho kikosi cha timu hiyo kitaingia kambini na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi,  Kurasini, jijini Dar es Salaam, kujiandaa na mtanange huo wa kukata na shoka.

“Kesho tutaingia kambini na kufanya mazoezi asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, lengo letu ni kutaka kushindana,’’ alisisitiza Zahera.

Kwa upande wake, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo na hawategemei kupoteza, kwani mbio zao za kupigania ubingwa ziko pale pale.

“Tunajua kila tunapokutana na Azam mechi inakuwa ngumu, lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu ili kuendelea kujiweka katika mbio za ubingwa,” alisema Hafidh.

Yanga inaingia kwenye pambano hilo ikiwa inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kujikusanyia pointi 74 katika michezo 32, Azam ikiwa nafasi ya pili na pointi 66, baada ya kucheza mechi 31, watani zao, Simba wakijikusanyia pointi 60 baada ya michezo 23.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*