YANGA WAIBEBA LIPULI KUIFUNGA SINGIDA UNITED

NA WINFRIDA MTOI    |   

KOCHA Mkuu wa Lipuli FC, Amri Said, amesema wamefanikiwa kuifunga Singida United baada ya kutazama video za mechi ya timu hiyo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga.

Lipuli waliifunga Singida bao 1-0 juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa na kukifanya kikosi hicho kufikisha pointi 31, kikiwa nafasi ya saba kwa kucheza michezo 25.

Akizungumza na BINGWA jana, Said, alisema ushindi huo umewafanya kulipa kisasi kwa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Hans Pluijm, kwa sababu mchezo wa kwanza waliwafunga bao 1-0, Uwanja wa Namfua, Singida.

Alisema kabla ya mechi, benchi la ufundi lilikaa na kupanga mikakati ya kushinda nyumbani na kuona njia mojawapo ni kuangalia video za mechi za wapinzani wao na kuwaweka sawa wachezaji kisaikolojia.

“Singida ni timu nzuri, ina kocha bora lakini tuliingia uwanjani tukiwa kumeshazisoma mbinu za Hans (Pluijm), kwenye video za mechi waliyocheza na Yanga na ile tuliyocheza nao mzunguko wa kwanza na kweli hakubadilika,” alisema.

Alieleza kuwa baada ya mapumziko ya siku moja, leo wanaanza mazoezi ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya Simba, itakayochezwa Ijumaa, Iringa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*