YANGA WAHAHA KUMBAKIZA YONDANI

NA HUSSEIN OMAR   |    

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ikielekea ukingoni, uongozi wa Yanga umesema umejipanga kuhakikisha unafanya kila linalowezekana kumbakisha beki wake wa kati, Kelvin Yondani ‘Vidic’.

Yondani amemaliza mkataba na anachokifanya sasa ni sawa na kucheza kwa makubaliano maalumu, ambayo kwa lugha ya kijiweni wanasema ‘deiwaka’.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, amesema wamejipanga kuhakikisha wanampa mkataba mnono Yondani, ambao utamfanya aendelee kufurahia maisha yake katika klabu hiyo ya Jangwani.

Akizungumza na BINGWA, Mkwasa, alisema mkataba wa Yondani utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu na uongozi tayari umejipanga kufanya kila linalowezekana ili kumbakisha nyota huyo.

“Wataondoka wote lakini si Yondani, ni mtu muhimu sana kwetu, tumejiridhisha kwa kila hali, ana mapenzi makubwa na timu lakini pia amekuwa ni mmoja wa wahamasishaji wazuri kwa wenzake uwanjani,” alisema Mkwasa.

Kwa upande wake Yondani alisema mkataba wake na Yanga umemalizika tangu Desemba mwaka jana na anachokisubiri ni kumalizika kwa msimu ndipo mazungumzo ya mkataba mpya yaanze.

“Nimemaliza mkataba wangu lakini nimekuja Yanga kufanya kazi, nawasikiliza viongozi mimi sina maneno mengi, ukizingatia muda unakwenda kasi,” alisema Yondani.

Yondani ambaye wengi wanamfahamu kwa uwezo wake wa kucheza mipira ya juu, alisema kinachompa jeuri ni kucheza kwa kujituma na kujitunza ndiyo maana ameweza kucheza soka la ushindani kwa muda mrefu.

Aidha, mlinzi huyo alidai katika kipindi hiki ambacho umri unaelekea kumtupa mkono, amejipanga vema kimaisha kwa kuhakikisha anapewa mkataba mnono utakaokidhi matakwa yake.

“Sikufichi, natakiwa nijipange ili baadaye niishi kama mfalme, nisije kudhalilika, nasubiri hao viongozi ili tuanze mazungumzo mimi sina noma wao tu,” alisema.

Akilizungumzia hilo la Yondani, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alisema mbali na mchezaji huyo, pia Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Obrey Chirwa, Goeffrey Mwashiuya na Beno Kakolanya, nao wamemaliza mikataba yao, lakini wanapaswa kusubiri msimu wa ligi umalizike.

“Hao wachezaji wote waliosema wamemaliza mikataba hawana budi kusubiri mpaka msimu wa ligi umalizike ndipo mazungumzo yaanze,”                              alisema Ten.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*