Yanga: Tuna kazi mbili J’mosi

NA WINFRIDA MTOI

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuondoka leo kuelekea Iringa tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Lipuli FC ya huko, huku viongozi na mashabiki wa Wanajangwani hao wakiweka wazi kuwa na vibarua vizito viwili wikiendi hii.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Samora, unatarajiwa kuwa na upinzani wa hali ya juu ambapo ushindi pekee ndio lengo la Yanga ili iweze kuendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo.

Yanga watapepetana Jumamosi jioni na Lipuli wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata msimu uliopita kwenye uwanja huo, ikiwa ni baada ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Saalam.

Msimu huu, Yanga ilianza kwa kuipa Lipuli kichapo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, bao hilo pekee la ushindi likifungwa na Heritier Makambo.

Pia, Yanga wanakwenda Iringa wakiwa wametoka kushinda mechi iliyopita kwa kuifunga timu inayoaminiwa kuwa ngumu kati Ligi Kuu Bara, KMC waliyoichapa mabao 2-1.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 67, baada ya kucheza mechi 27, ikishinda 21, sare nne na kupoteza mbili.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, ameliambia BINGWA kuwa tayari wamemaliza maandalizi baada ya kufanya mazoezi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

Alisema jana walifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini na kuingia kambini katika Hoteli ya Nefaland iliyopo Manzese, Dar es Salaam kujiandaa na safari ya Iringa.

“Leo (jana) tulikuwa na mazoezi ya kuwekana sawa na kushambulia pekee ikiwa ni kurekebisha makosa na kuwafanya wachezaji kutumia vizuri nafasi kufunga mabao,” alisema Mwandila.

Mwandila alisema katika kikosi kinachoondoka watamkosa Abdallah Shaibu ‘Ninja’, anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Andrew Vincent ‘Dante’ ambaye ni majeruhi.

Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Ibrahim Ajib, aliweka bayana mikakati yao kuelekea mchezo huo kuwa ni kuchukua pointi tatu kwa Lipuli kama walivyofanya mechi iliyopita.

Ajib alisema huu ni wakati wao wa kukusanya pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupigania ubingwa, licha ya kikosi chao kuonekana hakitaweza.

“Katika mchezo huu tutamkosa Ninja, pengo lake lipo lakini tunajua jinsi ya kujipanga kupata matokeo kwa wale tutakaofanikiwa kuwepo,” alisema.

Ajib alisema mchezo huo utakuwa mzuri na wa kuvutia ikiwa ni njia ya kutoa burudani kwa mashabiki wao waliopo Iringa na mikoa ya jirani.

Katika hatua nyingine, mashabiki na wapenzi wa Yanga wameeleza jinsi walivyojipanga kwa siku ya Jumamosi kwa kuisapoti timu yao, huku wakiwa na kazi nyingine ya nyongeza ya kuwaombea mabaya watani wao wa jadi, Simba ili wapoteze mchezo wao dhidi ya AS Vita ya DR Congo.

Mchezo huo ni wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwamba iwapo Simba itashinda, itakuwa imetinga robo fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi D.

Mwenyekiti Msaidizi wa tawi la Yanga la Wakali wa Temboni, Junior Mayswana, alisema wanatarajia kuondoka Ijumaa kwenda Iringa, lakini baadhi yao watabaki Dar es Salaam kushuhudia kipigo cha Simba.

Mayswana alisema katika hali ya kawaida, walitakiwa kuishangilia Simba ili kusonga mbele na kutoa nafasi kwa timu nyingine za Tanzania kushiriki michuano hiyo mwakani, lakini kutokana na midomo ya watani zao hao inabidi waiombee mabaya tu ipoteze.

“Simba wana mdomo sana, tena wakishinda ndiyo tutaishi kwa shida mtaani, tunakwenda Iringa lakini wengine watabaki Dar es Salaam, kazi ni moja kuhakikisha Watani wanakufa ili wafunge midomo.

“Lipuli tunayokwenda kukutana nayo tunajua ni tawi la Simba, fitina zitakuwa nyingi ila timejiandaa kupambana nazo kwa sababu tayari wenzetu wametangulia tangu jana kuweka mipango sawa,” alisema.

“Adui yako siku zote mwombee njaa,  hatuwezi kuwashangilia kamwe, kwanza  wametupa jina sisi la kusema kituo kinachofuta Jangwani na kumwonyesha Kagere akitufunga halafu leo hii tuwashangilie? Taifa tunakwenda kuwashangilia Wacongo,” alisema Katibu wa Tawi la Yanga Kurasini, Mustapha Mohammed.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*