googleAds

Yanga tatizo lipo hapa

MWAMVITA MTANDA NA ASHA KIGUNDULA

BAADA ya kutoka suluhu na Coastal Union ya Tanga, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amesema kuwa amebaini tatizo lililopo ndani ya kikosi chake akiahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa ushirikiano na uongozi wa klabu hiyo.

Akizungumza na BINGWA jana, Eymael alisema kuwa japo bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bata na hata michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), lakini kunatakiwa kufanyika jambo ndani ya kikosi chake ili kufanikisha hilo.

“Wachezaji wana kila uwezo wa kuipa timu ushindi, lakini wanaonekana kutojiamini katika hilo, wapo wanaojituma na wengine wamekuwa wakishindwa kutimiza majukumu yao, ninalifanyia kazi hilo pamoja na wenzangu wa benchi la ufundi, lakini pia tutawashirikisha viongozi.

“Hatuna muda wa kupoteza, baada ya mechi ya Tanga, tumeshawasili Dar es Salaam na kuendelea na program zetu za mazoezi, nina imani mechi zijazo kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Eymael.

Mbelgiji huyo alisema, japo wana uwezo wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kama vijana wake wataamua, lakini akili yake kwa sasa inawaza taji la ASFC ili waweze kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Alisema ili kufanikisha hilo, wanajipanga kuhakikisha wanaitoa Gwambina FC katika michuano ya ASFC katika mchezo wa hatua ya 16 bora utakaopigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na hivyo kutinga robo fainali.

Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umepanga kufanya kikao maalum na wachezaji wao kujua tatizo linalosababisha kupata sare nne mfululizo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na BINGWA juzi, Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alisema wamekuwa wakishangazwa na matokeo hayo wakati wachezaji wao wanatimiziwa mahitaji yao.

Alisema kuwa kikao hicho kitafanyika haraka iwezekanavyo ili kuweka mambo sawa na ikiwezekana kikosi chao kurejesha moto wake.

“Ni jambo la kushangaza sana, wachezaji hawana tatizo, mahitaji yao wanatimiziwa, lakini tunapata matokeo yasiyoridhisha, inasikitisha sana. Tumepanga tukutane nao (wachezaji) pamoja na benchi la ufundi tujue tatizo gani linachangia,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*