Yanga, Simba kushitakiwa

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa Coastal Union ya Tanga, umepanga kuzishitaki Simba na Yanga baada ya kupata ushahidi wa kutosha wa klabu hizo kufanya mazungumzo na beki wao, Bakari Mwamnyeto.

Yanga inadaiwa kuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na Mwamnyeto tangu msimu uliopita kabla ya Simba kuingilia dili hilo, ikielezwa tayari wameshampa kifunga uchumba.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto, ameliambia BINGWA juzi kuwa Mwamnyeto amesalia na mkataba wa mwaka mmoja, hivyo Simba na Yanga kufanya mazungumzo naye wamekiuka kanuni za usajili.

“Tunakusanya ushahidi katika hili na hata mchezaji mwenyewe tumemwambia tukiupata tu, tutazishitaji timu zinazohusika kufanya mazungumzo naye.

“Mwamnyeto amesalia na mkataba wa mwaka mmoja na tulianza kufanya naye mazungunzo kwa ajili ya kumwongeza mwingine, hivyo hizo Simba na Yanga zifahamu hatumuuzi mchezaji wetu,” alisema.

Mguto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, alizitaka Simba, Yanga na timu nyingine kusubiri mkataba wa mchezaji huyo uishe ndipo zimsajili.

“Waendelee kumshawishi Mwamnyeto agome kuongeza mkataba mpya Coastal wakati wakisubiri alioana uishe ndipo wamchukue tofauti na hapo, hatumuuzi,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*