YANGA SI SAWA KUJITOA KOMBE LA KAGAME

NA CLARA ALPHONCE

MASHINDANO ya Klabu Bingwa  kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati maarufu ‘Kagame Cup’  yanayoandaliwa na  Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA),  yanatarajia kufanyika Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu, Dar es Salaam.

Wenyeji Tanzania watawakilishwa na timu za Klabu za Simba, Yanga na Azam  ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo.

Katika ratiba ya mashindano hayo  Simba na Yanga wamepangwa katika kundi moja, lakini kuna tetesi kwamba Wanajangani hao wamewasilisha barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka kujitoa kutokana na sababu mbalimbali. 

Viongozi wa Matawi wa Yanga  ndio waliopendekeza kwa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo  kuhusu timu yao kujitoa katika mashindano ya Kagame kwa sababu wanakabiliwa na mashindano  makubwa zaidi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga inajiandaa kukipiga na Gor Mahia ya Kenya Julai 18 mwaka huu, baada ya kucheza michezo miwili ya hatua ya makundi, huku wakiwa wamefungwa mmoja na kutoka sare mmoja.

Katika mchezo wa kwanza  wa kombe hilo dhidi ya USM Alger ya Algeria Yanga walipoteza ugenini kwa mabao 4-0, kisha kutoka suluhu na Sports Rayon ya Rwanda  katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Michezo hiyo miwili Yanga hawajafanya vizuri , na wanahitaji kufunga mkanda kweli kweli katika michezo iliyobaki ili waweze kupita katika kundi hilo, linalotoa timu mbili  kwenda robo fainali.

Yanga wanahitaji mechi nyingi za kirafiki ili iweze kufanya vizuri katika mashindano mikubwa, ingawa wanataka kutojitoa katika mashindano ya Kombe la kagame 

Mashindano ya Kombe ya Kagame yanaweza kutumika kwa Yanga  kama mazoezi ya kujiandaa  dhidi ya Gor Mahia, lakini kitendo cha kujitoa si sawa, kwani wamejenga uzoefu wa kimataifa.

 Michezo ambayo wangekuwa wanacheza  ingemfanya kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera,  kujua vizuri udhaifu wa kikosi chake na kujua jinsi gani ya kukifanyia marekebisho kikosi hicho kabla ya kuendelea na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 Kufanya mazoezi tu bila kupima kikosi chao sidhani kama ni njia sahihi ya kufanikiwa kwenye mashindano hayo ya kimataifa ya Afrika.

Yanga hawatakiwi kuyaogopa mashindano ya Kombe la Kagame na  wanachotakiwa ni  kupambana ili kupata matokeo mazuri na baadaye kuchukua ubingwa.

Kukataa mashindano hayo  kwa sababu ya kufungwa na Simba huo ni ushamba ambao hauna faida katika soka,  kwani mwanajeshi hawezi kuogopa vita na kufa vitani niushujaa.

 Pia itakuwa ni fursa kwa wachezaji kuonyesha viwango vyao katika mashindano ya Kombe la Kagame  ili wapate soko la  kusajiliwa na timu nyingine.

Naamini kwamba Yanga  wana  wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza timu kubwa zaidi  barani Afrika, hivyo uongozi wa klabu hiyo kuondoa timu katika Kombe la Kagame ni kuwanyima fursa.

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*