YANGA SC NYODO TUPU

>>Ushindi wa juzi wawapa kiburi mjini, wawabeza Simba

>>Watamba Chirwa, Yondani, Tshishimbi kumaliza kazi Ethiopia

NA WAANDISHI WETU

USHINDI wa mabao 2-0 walioupata Yanga katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia juzi, umewapa jeuri wapenzi wa timu hiyo mbele ya watani wao wa jadi, Simba.

Kutokana na kipigo hicho walichokitoa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga sasa watahitaji ushindi au sare ya aina yoyote dhidi ya wapinzani wao hao katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mara baada ya mchezo wa juzi, mashabiki wa Yanga walisikika wakiwatambia wenzao wa Simba, wakidai kuwa matokeo hayo yamewapa uhakika wa wachezaji wao kuendelea kupanda ndege, huku wale wa watani wao hao wakipigana vikumbo na Ndanda, Majimaji na nyinginezo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Habari ndiyo hiyo, mlikuwa mkitucheka kuwa kwa kikosi hiki hatuwezi kushinda leo (juzi) ndio maana mlikuja kwa wingi uwanjani kutuzomea…kwa wachezaji hao hao mnaowabeza, tumeshinda na mechi ya marudiano ‘chama’ (kikosi) litakuwa limekamilika, lazima tushinde na kusonga mbele,” alisikika akisema mmoja wa mashabiki wa Yanga nje ya Uwanja wa Taifa, huku akiungwa mkono na wenzake.

Tambo za mashabiki wa Yanga ziliendelea juzi na jana kwenye vyombo vya usafiri, maofisini na hata kwenye mitandao ya kijamii, zaidi wakijivunia kushinda bila kuwa na nyota wao kama Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Juma Said Makapu na Papy Tshishimbi ambao wanatumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Wengine walioukosa mchezo huo ni Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao ni majeruhi, wakiwa ni wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza.

Akizungumzia mchezo huo, Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema siri ya ushindi wao ni nidhamu, kujituma, kiu ya mafanikio na kufuata maelekezo ya makocha wao.

“Mchezo wa marudiano tutakuwa na wachezaji wetu wote kwani wale wanaotumikia adhabu ya kadi, watakuwa huru, hivyo matumaini ya kusonga mbele ni makubwa, mashabiki waendelee kutupa sapoti na watuombee,” alisema.

Hata hivyo, aliwapongeza wachezaji waliopambana kufa au kupona juzi na kupata ushindi huo dhidi ya Waethiopia hao ambao alisisitiza kuwa si wa kubezwa hata kidogo.

“Nyote mmeona, vijana waliopangwa leo (juzi), wamepambana hasa, binafsi ninawapongeza sana na tuendelee kuwaamini na kuwathamini,” alisema Cannavaro ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Vincent Andrew ‘Dante’ aliyeumia.

Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga imesema kuwa baada ya mchezo wao wa juzi, wameelekeza akili na nguvu zao zote kuelekea mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United keshokutwa.

Mchezo huo wa marudiano utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kutolewa na wapinzani wao hao kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania (Azam Confederation Cup) kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 1-1.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema wanachokitazama mbele yao ni kwa vipi washinde mchezo huo dhidi ya Singida United ambao wamekuwa wapinzani wao wakubwa.

“Tunajua tuna mechi kubwa mbele ya kimataifa, lakini kwanza macho yetu yameelekea katika mchezo dhidi ya Singida ambao ni muhimu kwetu kujipanga na kupata matokeo ambayo kwanza yatatufanya tuwe vizuri kwenye kutetea ubingwa wetu, lakini pia tuwe vizuri kwenye mechi ya marudiano na Welayta Dicha,” alisema.

Mkwasa alisema tayari kikosi cha Yanga kinaendelea kujinoa kuelekea katika mchezo huo wenye ushindani na upinzani mkubwa.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi kimepumzika jana ambapo leo kitaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

“Timu kwa ujumla ipo vizuri, hata Tambwe ambaye awali aliachwa Dar es Salaam na baadaye tukaungana naye Morogoro, anaendelea vizuri, kupangwa au kutokupangwa ni maamuzi ya mwalimu,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*