googleAds

YANGA NI MAFURIKO U/TAIFA LEO

NA ZAITUNI KIBWANA,

MASHABIKI wa Yanga leo wanatarajiwa kufurika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuona iwapo timu yao inaweza kuifunga Toto African ya Mwanza na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamebakiza pointi tatu kutetea ubingwa wao ambapo kwa sasa wamebakiza mechi mbili, ya leo na ile ya mwisho dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hadi sasa, Yanga wana pointi 65 baada ya kushuka dimbani mara 28, wakiwa kileleni mwa msimamo kutokana na idadi kubwa ya mabao, kwani wanalingana pointi na Simba iliyobakiza mchezo mmoja.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi uwanjani leo kuongeza hamasa kwa wachezaji wao kushinda mchezo huo ambao ni muhimu mno kwao.

“Tulikuwa na wakati mgumu sana katika mchezo wetu dhidi ya Mbeya City (Jumamosi iliyopita), waliweza kutubana na kuharibu mipango yetu yote. Lakini tunashukuru Mungu vijana walipambana na tukapata ushindi.

“Sasa kilichobaki ni kumaliza kazi kesho (leo) dhidi ya Toto, hivyo mashabiki waje kwa wingi uwanjani tuanze sherehe za ubingwa kwa pamoja,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*