googleAds

Yanga kujua mpinzani wake CAF leo

NA JESSCA NANGAWE

WAKATI droo ya mechi za mtoano kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ikitarajiwa kupangwa leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametamba kuwa ana kikosi imara kinachoweza kupambana na timu yeyote.


Yanga iliangukia hatua hiyo baada ya kutolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2, katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini.


Timu hiyo ilianza kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam , kabla ya kukubali kichapo cha bao 2-1 katika mchezo wa marudiano uliochezwa mjini Ndola, Zambia.


Wanajangwani hao wataanzia kampeni zao nyumbani katika mchezo utakaopigwa Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya kurudiana Novemba 3, mwaka huu ugenini.
Yanga inaweza kupangwa na timu za Paradou AC (Algeria), ESAE (Benin), DC Motema Pembe ( Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo) na FC San Pedro (Ivory Coast).
Nyingine ni Pyramids (Misri), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).
Zahera alisema,hana shaka kupangwa na timu yeyote kwenye michuano hiyo kwani anaamini ana kikosi bora kinachoweza kumpa matokeo mazuri na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Alisema baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika , kikosi chake kinaelekeza nguvu zote katika Kombe la Shirikisho, hivyo haoni timu itakayowazuia kuingia hatua ya makundi.
“Tunajua kesho (leo) tutajua mpinzani wetu kwenye mchezo wa mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, tunasubiri kwa hamu kumjua na baada ya hapo tutaanza mara moja maandalizi kuhakikisha tunashinda”alisema Zahera.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*