googleAds

Yanga ‘itabugi’ ikimtimua Pluijm

NA ERNEST CHENGELELA (OUT)

KUNA msemo maarufu kwenye soka unaosema makocha huajiriwa ili wafukuzwe na wenyewe wanajua hilo kuwa wakati timu yao inapokuwa na matokeo mabovu basi vibarua vyao huwa haviko salama kabisa.

Ndiyo maana hata makocha bora duniani kuna nyakati wamepitia kwenye janga la kutimuliwa, unaweza kuona watu kama akina Jose Mourinho, Carlo Ancelloti, Fillipe Scolari na wengine wengi wamewahi kuonja chungu ya kutimuliwa kutoka kwenye kazi zao.

Lakini, moja ya vitu ambavyo waajiri wengi huangalia kabla ya kumtimua kocha ni matokeo yake na iwapo kweli ameshindwa kabisa kuipigisha hatua timu yao.

Ila kwa Tanzania hali ni tofauti, kuna wakati mwingine kocha hutimuliwa kutokana na sababu za kiajabu ajabu kabisa ambazo ni aibu hata kuzitaja.

Sasa hivi kuna tetesi kuwa Yanga inataka kumfungulia milango ya kutokea kocha wake, Hans van der Pluijm, baada ya sare ya bao 1-1 ambayo timu hiyo iliipata dhidi ya watani wao wa jadi, Simba.

Inadaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa klabu hiyo wanaamini kuwa uwezo wa kocha huyo umefika tamati, hii ni kutokana na timu kuanza kwa kusuasua msimu huu, huku ikiwa imevuna pointi 11 katika mechi sita ilizocheza hadi sasa.

Ikiwa imeshinda mechi tatu, kutoka sare mbili na kufungwa moja matokeo ambayo yamewafanya wengi kuanza kumlaumu kocha huyo bila kujali kuwa ni yeye ndiye aliwapeleka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Lawama za baadhi ya wanachama na viongozi wa Yanga zinasahau kuwa Pluijm ndiye aliwapa mataji mawili msimu uliopita na kuifanya timu hiyo kutajwa kama moja kati ya klabu bora zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Wengi wanamhukumu zaidi kwa matokeo ya bao 1-1 ambayo Yanga iliyapata dhidi ya Simba kitu ambacho si sahihi hasa ukiangalia na ukweli kuwa soka ni mchezo wenye matokeo ya aina tatu, kushinda, kufungwa na sare.

Binafsi naamini Yanga wanatakiwa kukaa chini na kumpa sapoti yao yote Pluijm kwa sababu baada ya miaka mingi ya klabu hiyo kuongozwa na makocha kutoka nje ya Bara la Afrika ambao hawana ubora sana kwa Mholanzi huyo wamepata bonge la kocha.

Na ameifanya Yanga kuweza kuzitesa hata timu za Kiarabu pindi inapokutana nazo, hivyo badala ya kuendelea kumweka kwenye wakati mgumu kocha wao wanatakiwa kusimama nyuma yake kwa sababu tayari ameshathibitisha kuwa yeye ni kocha wa kiwango cha kimataifa kweli.

Mashabiki wanatakiwa kujua kuwa kinachoitesa Yanga kwa sasa si udhaifu au kufika mwisho kwa mbinu za Pluijm na benchi lake la ufundi, bali ni uchovu ambao umetokana na timu hiyo kukosa muda wa kupumzika wakati timu nyingine zikiwa mapumzikoni.

Hakuna asiyejua kuwa Yanga haikupata muda wa kupumzika wakati ligi ya msimu uliopita ilipoisha kutokana na kushiriki michuano ya Afrika, hivyo uchovu sasa umeanza kuwatesa wachezaji wake ambao kama binadamu wa kawaida wameuchoka mchezo wa soka.

Kila nikiangalia naamini kuwa Yanga itafanya kosa kubwa sana kumtema Pluijm kwa sababu si mara zote unaweza kupata kocha mwenye ubora wa Mholanzi huyo.

Yanga wanatakiwa kuangalia namna ambavyo watani wao wa jadi Simba wamekuwa wakipata shida sana kutafuta makocha bora kiasi cha kujikuta kila kukicha wakitimua timua makocha kutokana na kushindwa kufikia ubora wanaoutaka.

Hivyo, kumfukuza Pluijm kunaweza kuwarudisha kule kwa makocha wasio na vigezo ambao wataishusha timu chini badala ya kuipeleka mbele kutoka sehemu iliyoishia msimu uliopita.

Yanga wanatakiwa kujua faida ya kudumu na kocha kwa kipindi kirefu kwa sababu kwa kufanya hivyo wanakuwa na mtu ambaye anaweza kuja na mipango ya muda mrefu na kutimiza ndoto za timu hiyo kutikisa soka la kimataifa.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*