Yanga hesabu zimetiki

TIMA SIKILO

BAADA ya kufanikiwa kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kukabiliwa na ukata, Yanga inaamini hesabu zao zimetiki na sasa hakuna timu itakayoweza kuwazuia kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Mara baada ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara, kikosi cha Yanga hakikuwa kikipewa nafasi kubwa ya kutamba kutokana na kuwa na wachezaji wengi wa kawaida, huku mafundi wakiwa ni wachache mno.

Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda, kikosi cha timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, kiliendelea kufanya vizuri na kuwashangaza wengi.

Hadi sasa, Yanga ikiwa imecheza mechi 16, haijapoteza hatamoja zaidi ya kupata sare mbili tu, ikiwamo dhidi ya ‘matajiri’ Simba ambao kikosi chao kimesheheni wachezaji wa kiwango cha juu.

Baada ya kubaini kikosi chao ni cha kawaida sana, hesabu za Yanga zilikuwa ni kupambana kwa jasho na damu ili kuwa ndani ya timu tatu za juu, lakini hatimaye wamepita malengo yao hayo.

Akizungumzia hilo, Zahera alisema: “Hesabu zetu ilikuwa tuwe katika nafasi tatu za juu, tulijua hatuna kikosi cha ushindani kulinganisha nawapinzani wetu, Simba na Azam.

“Lakini kutokana na nidhamu na jitihada za wachezaji, tumefanikiwa kukaa juu ya msimamo wa ligi, tunajivunia sana kwa mafanikio haya si madogo.

“Tukijua kipindi cha dirisha dogo la usajili, tungepata wachezaji wa kiwango cha juu ili kuiongezea nguvu timu, lakini hilo limeshindikana, tumempata mmoja (Haruna Moshi ‘Boban’) ambaye naamini ataongeza kitu katika timu yetu.”

Zahera alisisitiza: “Kwa sasa hatuwezi kurudi nyuma, tutazidi kusonga mbele kwa kutumia mbinu na mipango ile ile iliyotufanya tuwe kileleni mwa ligi pamoja na wachezaji kuwa na matatizo ya kifedha baada ya kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu.

“Tunaamini katika umoja hakuna linaloshindikana, hesabu zilezile zilizotuweka kileleni mwa ligi, ndizo tutakazozitumia kutuwezesha kutwaa ubingwa wa ligi. Sidhani kama itakuwa ni kazi kubwa.”

Yanga hadi sasa imejikusanyia pointi 44 baada ya kushuka dimbani mara 16, ikiwa imeshinda mechi 14 na kupata sare mbili tu.

Azam waliocheza mechi 16, pia wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 40, baada ya kupata sare nne, lakini wakiwa hawajafungwa mchezo hata mmoja kama Yanga.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba, wanashika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 27 kutokana na mechi 12.

Previous Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*