Yanga haiachi kitu

NA HUSSEIN OMAR

YANGA wamepania kuondoka na pointi zote tatu leo watakapovaana na Lipuli FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa, ili kuendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo yenye timu 20.

Wanajangwani hao wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 67 walizovuna kutokana na mechi 27, sawa na Azam wanaowafuatia na pointi zao 56, wakati Simba wanashika nafasi ya tatu baada ya kuzoa pointi 51 ndani ya mechi 20.

Kuelekea mchezo huo wa leo, Yanga wamepania kufanya kweli kuendeleza wimbi la ushindi kutokana na maandalizi kabambe waliyofanya ili kuwaliza wenyeji wao hao.

Akizungumza na BINGWA jana, kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, alisema vijana wake wapo tayari kwa ushindi baada ya kufanyia kazi kasoro kadhaa zilizojitokeza katika michezo iliyopita.

“Kama unavyojua kesho (leo) tupo ugenini kucheza dhidi ya Lipuli, tumejiandaa vizuri licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wetu tegemeo, lakini waliopo wapo tayari kwa mchezo,’’ alisema Mwandila.

Yanga leo itawakosa nyota wao kama Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu, Andrew Vincent ‘Dante’ na Ibrahim Ajib ambao ni majeruhi.

Rekodi zinaonyesha kuwa msimu uliopita Yanga walipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora ikiwa ni baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Msimu huu Yanga ilianza kwa kuipa Lipuli kichapo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, bao hilo la pekee la ushindi likifungwa na Heritier Makambo.

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Yanga, Lipuli kupitia kocha wao msaidizi, Selemani Matola, wametamba kufanya kweli na kuchukua pointi zote tatu.

“Ni mchezo mgumu, lakini nina matumaini ya kushinda kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, kama unavyofahamu, ligi ipo katika hatua ya lala salama, hivyo hakuna anayetaka kufanya makosa na kupoteza mchezo kirahisi,’’ alisema Matola.

Katika msimamo wa ligi hiyo, wakati Yanga wakiwa kileleni na pointi zao 67, Lipuli wanashika nafasi ya sita wakiwa wamejikusanyia pointi 41 baada ya kushuka dimbani mara 30.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*