googleAds

YANGA, GSM FRESH

NA ZAINAB IDDY

KILA kitu sasa ni shwari Jangwani baada ya uongozi wa Yanga kumalizana na wadhamini wao, kampuni ya GSM Group iliyotangaza kujiweka pembeni kuisaidia klabu hiyo.

Mapema jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii na mingineyo, kulisambaa barua ya GSM kwenda kwa uongozi wa Yanga ikielezea nia ya kampuni hiyo kujitoa kusaidia mambo yaliyopo nje ya mkataba ndani ya Wanajangwani hao.

Barua hiyo ilizua taharuki miongoni mwa mashabiki, wanachama na hata wachezaji wa Yanga, hivyo kuja juu wakiutaka uongozi wao chini ya Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla kufanya kila wawezalo ili kunusuru ‘ndoa’ yao na GSM.

Wanachama wa Yanga katika matawi na ‘magroup’ mbalimbali ya Whatssap, walionekana kucharuka na kuujia juu uongozi wao wakihoji imekuwaje hadi wamewavuruga wadhamini wao hao.

Katika moja ya ‘magroup’, ilifikia hatua hadi Dk. Msolla akajitoa (left) baada ya kuandamwa na wanachama wa klabu hiyo, wakimshutumu kwa uongozi wake kuchangia hilo kutokana na majungu ya baadhi ya mabosi wa klabu hiyo.

Huko kwenye matawi jana ilikuwa ni mshike mshike, kwani habari za kujitoa kwa GSM zilikuwa ni kama mwiba mchungu kwao na kuamua kukutana haraka iwezekanavyo kuona nini cha kufanya.

Mwenyeki wa Mtawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Mhezi, aliliambia BINGWA kuwa viongozi wa matawi ya mkoa huo walipanga kukutana leo kuangalia namna bora ya kuifanya timu yao kuepukana na misuguano, ukiwamo uliowafanya GSM kujiweka pembeni.

“Leo (jana) tumeambiwa kamati (ya utendaji) imekutana, tunasubiri tamko lao baada ya ukimya mrefu, lakini kesho (leo) nasi tutakuwa na kikao cha dharura cha viongozi wa juu wa matawi tu ya mkoa huu kujadili namna ya kuwadhibiti wale wenye nia mbaya na Yanga,” alisema.

Ndani ya kikosi cha Yanga, wachezaji nao hawakuwa nyuma kusikitishwa na uamuzi huo wa GSM, wakiamini ungewaathiri mno.

Wakizungumza na BINGWA jana, wachezaji nyota wa timu hiyo, wakiongozwa na Said Juma Makapu, waliwataka viongozi wao kukutana na mabosi wa GSM kumaliza tofauti zao.

“Kwa kweli sisi kama wachezaji, tunatamani kuona mambo yanakuwa shwari ndani ya klabu yetu, tunaamini kwa hili lililotokea, uongozi wetu makini chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla na bosi Mwakalebele (Frederick-Makamu Mwenyekiti), utalimaliza tu.

“Ila nitoe rai kwa Wanayanga, tuepukeni na chokochoko zinazolenga kutugawa. Hakuna asiyefahamu kuwa GSM wamekuwa wakitusaidia kwa mengi, kwa sasa ari ya timu ipo juu kutokana na kazi kubwa inayofanywa na GSM kwa kushirikiana na uongozi.

“Tumeona kilichotokea katika mechi yetu na Simba tuliyoshinda kwa bao 1-0, GSM walichangia kwa kiasi kikubwa kutokana na hamasa waliyotupa sisi wachezaji. Tunaomba GSM waheshimiwe,” alisema Makapu akiungwa mkono na nyota wengine wa klabu hiyo. 

Habari zilizopatikana jioni jana, zinasema kuwa uongozi wa Yanga uliitisha kikao kilichoanza saa saba mchana hadi saa 11 jioni.

Mbali ya Dk. Msolla na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji, kikao hicho pia kilihudhuriwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia BINGWA kuwa Mavunde alichukua jukumu la kuwaita mezani wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na wawakilishi wa GSM ili kumaliza sakata hilo kwa maslahi mapana ya timu.

“Hali ilishakuwa mbaya, baadhi ya wanachama walitoa siku mbili kwa Mwakalebela na Msolla kulimaliza suala hilo au kujiudhulu, ndipo mheshimiwa Mavunde alipoamua kuingilia kati.

“Shukrani nyingi ziende kwa Mavunde aliyeziita pande hizo mbili na kuzungumza nazo kisha GSM wakapewa baraka zote kuendelea na majukumu waliyokuwa wakifanya na Msolla amewahakikishia kuwa uongozi wake utaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nao bega kwa bega,” alisema mtoa habari huyo ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

BINGWA lilimtafura Msolla ambaye hakutaka kuzungumza mengi na badala yake, alisema: “Kila kitu kipo sawa, wanachama wawe watulivu, hakuna kitakachoharibika kwa sababu wote tuna nia moja ya kuijenga Yanga.”

Lakini nini chanzo cha sakata hilo?  

Baada ya mshambuliji wa timu hiyo, Bernard Morrison kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na kupiga picha na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mkandarasi Hersi Said, baadhi ya wajumbe wa kamati  za Yanga walihoji uhalali wa wadhamini wao hao kufanya kazi ambazo zilipaswa kufanywa na viongozi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya Yanga, wajumbe waliodaiwa kuhoji jambo hilo katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, ni Rodgers Gumbo, Salim Rupia na Shija Richard.

Wajumbe hao walihoji inakuwaje GSM inafanya usajili bila kuitaarifu Kamati ya Utendaji, wakati si sehemu ya makubaliano katika mkataba wao na Yanga, jambo lililozua taflani ndani ya kikao.

Kutokana na sekeseke hilo, ndipo jana GSM walipoandika barua na kuwapelekea Yanga, wakieleza uamuzi wao wa kusitisha utekelezaji wa masuala yaliyo nje ya mkataba na klabu hiyo.

Kwa mujibu barua hiyo, kampuni hiyo imekuwa ikisajili wachezaji, ikigharamia kambi, uwanja wa mazoezi, tiketi za ndege kwa benchi la ufundi na wachezaji, majukumu ambayo hayakuwa ndani ya mkataba wao bali kwa mapenzi tu.

Itakumbukwa kuwa GSM waliingia Yanga wakiwa na jukumu la kusimamia jezi (utengenezaji na usambazaji), pia kuitumia timu hiyo kunadi magodoro yao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*